Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKATI serikali ikiwataka viongozi wake katika
Halmashauri mbalimbali hapa nchini kufanya kazi kwa uwazi na kufuata taratibu
husika, hali hiyo imekuwa kinyume kwa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo
inadhihirisha pale agizo lililotolewa na Kaimu Afisa elimu msingi wa wilaya
hiyo, Alphonce Mwamwile juu ya michango wanayochanga wazazi kwa ajili ya
kuendeshea mitihani ya kata na shule mwishoni mwa mwezi na kuingizwa kwenye
akaunti ya Rukwa Computer Training Centre, imezua mapya kufuatia baadhi ya
Madiwani na Wenyeviti wa shule za msingi wa wilaya hiyo, kudai kuwa hakuna
kikao kilichoketi na kujenga makubaliano kwamba fedha hizo zipelekwe huko.
Madiwani na wenyeviti hao walidai kwa nyakati
tofauti kuwa, hata mchakato wa zabuni haujafanywa juu ya kumpata mzabuni huyo
ambaye hafahamiki ni wa kutoka mkoa au wilaya gani na amepewa jukumu la kuchapa
mitihani ya watoto wao, badala yake wanashangaa kuona waratibu elimu kata na
walimu wakuu mashuleni wakiagizwa kukusanya michango hiyo na kuiingiza kwenye
jina la akaunti hiyo.
Imeelezwa kuwa agizo hilo lililotolewa na Ofisa
elimu huyo linatekelezwa baada ya kuagizwa na Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri hiyo, Hussein Ngaga kwamba afanye hivyo na fedha ziingizwe kwenye
jina la akaunti hiyo jambo ambalo wamesema, kitendo hicho ni wizi wa fedha za
wananchi hivyo ni vyema zikafuatwa taratibu husika za kumpata mzabuni kwa
kufuata taratibu zenye uwazi na sio vinginevyo, hivyo kutozingatia hilo ni
kukosa utawala bora na kuleta migogoro isiyokuwa ya lazima katika jamii.
Mwandishi wa habari hizi amefanikiwa kupata barua
yenye kumbukumbu namba W/E/MB/10/VOL.111/66 ya Januari 15 mwaka huu, ambayo
inawaagiza waratibu na walimu wakuu wote shule za msingi wilayani Mbinga,
kukusanya michango hiyo ya wazazi kwa ajili ya kuendeshea mitihani hiyo na
kuiingiza kwenye akaunti namba 62101600263 benki ya NMB, ambayo
ni ya Rukwa Computer Training Centre.
Sehemu ya barua hiyo inaagiza kwamba itafanyika
mitihani sita ya wilaya kwa darasa la saba mwaka huu, mitihani minne fedha
zitatoka kwa wananchi na miwili itatoka kwenye akaunti ya Capitation Grant,
hivyo mwanafunzi mmoja kwa mtihani mmoja anapaswa kuchangia shilingi 1,500 kwa
masomo ya Hisabati, Kiswahili, Sayansi, Historia, Uraia, Jiografia na
Kiingereza.