Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KUFUATIA kudaiwa kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za mapato
yatokanayo na uvunaji wa msitu wa Mbambi uliopo katika kata ya Matarawe
Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani
humo Cosmas Nshenye naye ameapa akisema kuwa Ofisi yake itachukua hatua kali za
kisheria ikiwemo kulifanyia uchunguzi jambo hilo na kulifikisha kwenye vyombo
husika vya kisheria.
Nshenye alisema yeye binafsi hakubaliani na hali hiyo kwani
dhahiri inaonesha kuwa kumekuwa na vitendo viovu ambavyo vinatia shaka juu ya
mwenendo wa uvunaji wa msitu huo kwani ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu
husika bila kufuata miongozo ya serikali umefanyika.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga alisema hayo juzi alipokuwa
akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji huo
kilichofanyika mjini hapa, baada ya kuibuka hoja ya kumtuhumu Afisa misitu wa
mji huo David Hyera kuwa anadaiwa kwa namna moja au nyingine kushiriki katika
ubadhirifu wa mapato hayo.