Wednesday, March 26, 2014

MENEJA TANROAD RUVUMA AKALIA KUTI KAVU ANYOSHEWA KIDOLE MBELE YA BOSI WAKE

Msafara wa magari ziara ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma, ukiwa umekwama katika kijiji cha Mahenge wilayani Mbinga mkoani humo, wakati ukielekea leo katika kata ya Litembo.

Jitihada zikiendelea kunasua gari moja baada ya jingine katika msafara wa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu baada ya kukwama kwa muda wa saa moja, leo katika kijiji cha Mahenge ukielekea kata ya Litembo wilayani Mbinga. (Picha zote na gwiji la matukio Ruvuma)

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

DIWANI wa kata ya Litembo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Altho Hyera amemtuhumu Meneja wa wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani humo, Abraham Kissimbo kwamba amekuwa kiongozi mwenye kauli zisizoridhisha ambazo hazionyeshi uadilifu kama mtumishi wa umma.

Hyera alisema hali hiyo ilimkuta wakati alipokwenda ofisini kwake kupata ufafanuzi juu ya maendeleo ya ujenzi wa barabara yenye kilometa 26 kutoka Mbinga mjini kwenda Litembo, ambayo hivi sasa ina hali mbaya kutokana na magari kushindwa kupita katika kipindi hiki cha masika.

Diwani huyo alimnyoshea kidole Injinia Kissimbo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika katika kata hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa leo alikuwa katika ziara yake ya kikazi kutembelea kata ya Litembo kwa lengo la kujionea kero hiyo ya barabara ambayo malalamiko yake yamedumu kwa miaka mingi.


Alieleza kuwa Injinia huyo alikuwa akimweleza kwamba barabara hiyo hawezi kuishughulikia kwa sababu haina hadhi na kwamba zipo barabara ambazo hata kama akiamshwa usiku wa manane atazipatia kipaumbele.

“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa Meneja wa TANROADS alikuwa akiniambia kwamba, “barabara hii hawezi kuishughulikia kwa sababu haina hadhi, zipo barabara ambazo hata akiamshwa usiku wa manane yupo tayari kuzipatia kipaumbele”, alisema Hyera.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Mwambungu aliagiza barabara hiyo kufanyiwa matengenezo haraka huku akifafanua kwamba mkandarasi wa kuifanyia matengenezo tayari amekwisha patikana.

“Barabara hii naagiza iimarishwe ijengwe kwa kiwango kinachotakiwa, nataka wakati wote masika na kiangazi magari na wananchi wapite bila shida”, alisema Mwambungu.

Awali wakati magari ya msafara wa Mkuu huyo wa mkoa yakielekea katika kata hiyo ya Litembo majira ya asubuhi ulikumbwa na matatizo, baada ya magari hayo kukwama kwa muda wa saa moja katika kijiji cha Mahenge kilichopo katani humo kutokana na barabara hiyo inayolalamikiwa kuwa na hali mbaya.

Hata hivyo ililazimika watu waliokuwa ndani ya magari hayo kushuka na kupisha madereva, kufanya kazi ya kuyanasua ili yaweze kupita katika eneo hilo korofi na baadaye kuendelea na ziara.







No comments: