Saturday, March 29, 2014

JESHI LA POLISI MKOANI RUVUMA LAWATAKA ASKARI WAKE KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Akili Mpwapwa upande wa kulia akizungumza na wadau mbalimbali (hawapo pichani) katikla ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, juu ya dhana ya ulinzi shirikishi na kuwataka askari wake na wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kuepukana na vitendo vya uhalifu ambavyo vinahatarisha usalama wa raia na mali zao.

Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Godfrey Ng'humbi, akisisitiza jambo juu ya kuitaka jamii na Wadau mbalimbali wilayani Mbinga kushirikiana kwa pamoja katika kuendeleza masuala ya ulinzi shirikishi. (Picha zote na gwiji la matukio Ruvuma)









Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limesema Serikali kamwe haitavumilia kuona askari wake wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu, badala yake itahakikisha kwamba inachukua hatua mara moja kwa yule anayekiuka maadili ya utumishi wa umma ili kuwafanya wananchi na mali zao wanaishi katika hali ya usalama. 

Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Akili Mpwapwa alipokuwa katika ziara yake ya kikazi akizungumza na askari polisi na wadau mbalimbali wa mkoa wa Ruvuma, kwa lengo la kusisitiza juu ya uimarishaji wa ulinzi shirikishi.

Mpwapwa alisema lengo la ziara hiyo ni kutaka kutambua maeneo yake ya kazi, kubaini uhalifu, vikundi vya ulinzi shirikishi na wadau ambao wamekuwa wakichangia jeshi la polisi katika kuleta ufanisi wa masuala ya ulinzi katika maeneo yao. 


“Ndugu zangu serikali ipo katika kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kazi katika hali ya usalama, nawaomba wananchi na askari polisi wa mkoa huu jengeni ushirikiano katika kuimarisha ulinzi ili tuepukane na machafuko mbalimbali ambayo yanahatarisha usalama wetu”, alisema Mpwapwa.

Alisema jukumu la ulinzi ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele wakati wote kuanzia ngazi ya kitongoji, mtaa, kata mpaka katika maeneo ya mjini, ili wananchi waweze kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za kimaendeleo bila kupata usumbufu wa aina yoyote ile.

Hata hivyo alieleza kuwa katika kufanikiwa hilo ni lazima vikundi vya ulinzi shirikishi viimarishwe huku akifafanua kuwa suala la ulinzi halina itikadi ya chama au dini bali ni jambo ambalo sote tunapaswa kushirikiana kwa moyo mmoja.




No comments: