Monday, March 10, 2014

WANAWAKE MKOANI RUVUMA WALALAMIKIA UKATILI UNAOSABABISHWA NA HISIA ZA KIMAPENZI

Kutoka kulia ni Diwani wa viti maalum tarafa ya Mbinga mjini, Grace Millinga akifurahia jambo pamoja na Wanawake wenzake kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani, ambazo mkoani Ruvuma zilifanyika katika kijiji cha Kihereketi wilayani Mbinga.


Akina mama wa mkoa wa Ruvuma, wakiendelea kwa pamoja kufurahia maadhimisho ya sherehe za siku ya mwanamke Duniani.

Joseph Mkirikiti Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, akipokea maelezo mafupi kutoka kwa mjasiriamali ambaye anatengeneza kinywaji cha asili aina ya "Wine". {Picha zote na Gwiji la matukio Ruvuma}


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WANAWAKE mkoani Ruvuma wamelalamikia na kupinga vikali vitendo vinavyoendelea kushamiri, ambavyo hufanyiwa miongoni mwao mkoani humo ikiwemo ukatili, kupigwa na kuuawa kutokana na hisia za kimapenzi.

Aidha wamesema kuwa upande wa watoto wa kike kumekuwa na ukosefu wa usawa katika kupata elimu, hivyo kusababisha watoto wengi kuishi katika mazingira hatarishi.

Kilio hicho kilitolewa na Wanawake hao kupitia risala yao iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, katika sherehe za maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake duniani kilichofanyika katika mkoa huo kijiji cha Kihereketi kata ya Nyoni wilayani Mbinga.

Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya wanawake wenzake, Cosma Mbawala ambaye ni mkazi wa kijiji hicho alisema wanawake ni kichocheo kikubwa katika harakati za kuleta maendeleo lakini inasikitisha kuona wamekuwa wakinyanyaswa na kunyimwa haki zao za msingi.


Mbawala alifafanua kuwa kundi hili limekuwa pia likitengwa katika kushiriki kwenye maamuzi mbalimbali, ikiwemo uwiano na ugawanaji sawa wa rasilimali muhimu.

Alisema katika kukabiliana na matatizo hayo, ni wakati sasa kwa serikali kutupia jicho namna ya kupambana na hali hiyo ili kumpunguzia mzigo mwanamke na kumpa muda zaidi wa kushiriki katika kupanga na kusimamia mipango ya kimaendeleo.

“Serikali isimamie na kukemea vitendo viovu vinavyofanyika katika jamii hasa udhalilishaji kama vile ubakaji, unyanyapaa na ukatili wa aina nyingine ambao tunafanyiwa dhidi yetu”, alisema.

Hata hivyo kwa upande wake Mgeni rasmi wa sherehe hizo Mkirikiti aliiasa jamii iachane na vitendo hivyo vya ukatili kwa kuhakikisha kwamba, haki sawa kwa mwanamke zinazingatiwa huku akilinyoshea kidole kundi la Wanaume ambalo ndilo kinara wa vitendo hivyo.

Mkirikiti alisema ni vyema jamii ikaona umuhimu wa thamani ya mwanamke ikiwemo kuwashirikisha katika mambo muhimu ya kimaendeleo hususan elimu na sio kuwatenga au kufanya ubaguzi kwa namna moja au nyingine.


No comments: