Wednesday, March 26, 2014

MWAMBUNGU AUTAKA UONGOZI WA WILAYA KUCHUKUA HATUA ZA HARAKA KUNUSURU CHANZO CHA MAJI KIGONSERA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga (Aliyesimama) akisoma taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ambaye amekaa upande wa kushoto, amevaa suti nyeusi. (Picha na Kassian Nyandindi)



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ameutaka uongozi wa wilaya ya Mbinga mkoani humo, kuchukua hatua mapema ya kunusuru hali ya chanzo cha maji kilichopo kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera, ambacho kimevamiwa na watu wachache ambao huendesha shughuli za kilimo.

Aidha watu hao wameweka makazi karibu na chanzo hicho kwa kujenga nyumba za kuishi jambo ambalo linahatarisha kupotea kwa uoto wa asili katika chanzo.

Mwambungu alitoa agizo hilo alipokuwa wilayani humo katika ziara yake ya kikazi, mara baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya wilaya ambayo ilisomwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga.

“Hili jambo tusilifumbie macho, tuchukue hatua sasa kwa kuhakikisha wale watu wanahamishwa haraka ili kuweza kunusuru usalama wa chanzo kile”, alisema.


 Awali Mkuu huyo wa mkoa aliuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuhahakisha kwamba wanaendelea kuelimisha wakulima juu ya uzingatiaji wa kilimo bora cha zao la kahawa, ili waweze kuzalisha kwa ubora na hatimaye wapate bei nzuri katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa serikali imejipanga pia namna ya kukabiliana na ununuaji wa mahindi ya wakulima, hususani katika maeneo ambayo huzalishwa kwa wingi.

No comments: