Wednesday, April 2, 2014

WANAFUNZI WAPIGA MKUU WA SHULE NA KUSABABISHA UHARIBIFU WA MALI, SHULE YAFUNGWA KWA MUDA



Na Kassian Nyandindi,

Songea.

WANAFUNZI wa shule ya sekondari ya Village School of Tanzania (VST) iliyopo katika kijiji cha Unango wilayani Mbinga  mkoa wa Ruvuma wamefanya fujo kwa kumpiga  mkuu wao wa shule, na kuvunja baadhi ya samani za shule  hiyo huku wakisababisha  uharibifu mkubwa wa mali za shule na walimu wao.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Akili Mpwapwa  alisema kuwa  tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita majira ya saa za usiku katika kijiji hicho.

Alisema kuwa siku hiyo ya tukio  wanafunzi wa kidato cha tatu na nne  wa shule hiyo walifanya fujo na kusababisha mali za shule pamoja na za walimu wao kuharibiwa  ambapo nyumba mbili za walimu  zilivunjwa milango na madirisha.

Wanafunzi  hao walivunja kompyuta na kuchana  vitabu mbalimbali  na nguo za walimu wao na kusababisha fedha shilingi milioni mbili kupotea.


Uharibifu huo wa miundombinu ya shule pamoja na mali imeelezwa kufikia thamani ya shilingi milioni 17,680,000 na kwamba bado uongozi wa shule unaendelea  kuangalia hasara zaidi zilizojitokeza.

Kamanda Mpwapwa alibainisha kuwa sababu ya wanafunzi hao kufanya vurugu shuleni hapo ni kwamba mkuu wa shule hiyo Angelo Malaki  aliwazuia kufanya sherehe za kuwakaribisha  wanafunzi wenzao wa kidato cha kwanza,  wakati tayari walishachangishana  fedha  ambazo  walimkabidhi mkuu huyo wa shule kwa ajili ya maandalizi ya sherehe hiyo.

Kufuatia kwa vurugu hizo imelazimika  uongozi husika wa shule hiyo kuifunga kwa muda wa wiki mbili na wanafunzi wote wamerudishwa majumbani kwao, kupisha uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo na mpaka sasa hakuna mwanafunzi yoyote anayeshikiliwa na polisi.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya VST ambao majina yao waliomba yahifadhiwe walisema kabla ya kutokea vurugu hizo  wanafunzi walichangishana fedha shilingi laki saba,  kwa ajili ya  sherehe fupi za kuwakaribisha wanafunzi wenzao wa kidato cha kwanza na fedha hizo alikabidhiwa mkuu wa shule Angelo Malaki na walipomtaka mkuu wa shule apange tarehe ya kufanya sherehe hizo aliwalazimisha wafanye  katikati ya wiki wakati wanafunzi wenyewe walitaka wafanye siku ya jumamosi, ambayo mkuu huyo wa shule alikataa kwa madai kuwa yeye ni msabato hawezi kuruhusu shughuli hiyo ifanyike siku hiyo jambo ambalo lilianza kuzua mvutano.

Kwa upande wake  Mkuu wa wilaya ya Mbinga  Senyi Ngaga amethibitisha  kutokea kwa vurugu hizo na kusema hatua za awali zimeanza kuchukuliwa, kupitia vikao mbalimbali vya kamati ya shule pamoja na kamati ya maendeleo ya kata hiyo  ili kuweza kupata ufumbuzi wa chanzo cha vurugu hizo.

No comments: