Tuesday, April 8, 2014

BENKI YA NMB YAENDELEA KUTOA MSAADA, YASISITIZA WANANCHI KUFUNGUA AKAUNTI

Timu ya uongozi wa benki ya NMB, katikati ni Meneja wa Kanda ya kusini Lillian Mwinula (aliyeketi kutoka upande wa kulia) na aliyesimama ni Meneja wa benki hiyo tawi la Litembo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma Victor Msoffe wakiwa wamewasili katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi, ambaye ameketi upande wa kushoto. Wa kwanza kutoka kulia ni Mganga Mkuu wa wilaya hiyo John Papalika.

Mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi (katikati) akipokea msaada wa vyandarua na mashuka ya kulalia wagonjwa katika hospitali ya wilaya hiyo, kutoka kwa Meneja wa NMB Kanda ya kusini Lillian Mwinula.

Meneja wa benki ya NMB Kanda ya kusini Lillian Mwinula, akizungumza na uongozi wa hospitali ya Nyasa (hawapo pichani) wakati wa makabidhiano ya vyandarua na mashuka ya kulalia wagonjwa katika hospitali hiyo. Kutoka kulia ni Meneja wa NMB tawi la Litembo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma Victor Msoffe. (Picha zote na Gwiji la matukio Ruvuma)
Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

ZOEZI la utoaji wa mashuka na vyandarua katika Hospitali ikiwa ni lengo la kuwasaidia wagonjwa waweze kuwa na mazingira mazuri ya kulala pale wanapolazwa wodini, leo limeendelea kufanyika wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, ambapo benki ya NMB hapa nchini kupitia tawi lake la Mbinga imetoa msaada huo wilayani humo.

Jumla ya mashuka 30, vyandarua nane na foronya 30 vimetolewa na benki hiyo na kukabidhi kwa uongozi wa hospitali ya wilaya hiyo huku makabidhiano hayo yakishuhudiwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Ernest Kahindi.

Wilaya hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto lukuki katika sekta ya afya ikiwemo uhaba wa majengo ya kutolea huduma hiyo muhimu vilevile  magodoro, mashuka na mablanketi ya kulalia wagonjwa zinahitajika jitihada za makusudi zifanyike kwa haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo.


Meneja wa NMB Kanda ya kusini Lillian Mwinula akizungumza wakati wa kutoa msaada huo, aliushauri uongozi wa wilaya ya Nyasa kuona namna ya kuandika maombi kwa benki hiyo ili waweze kusaidiwa tena pale wanapoona wamekwama vifaa vya aina mbalimbali, ambavyo ni muhimu katika kuhudumia wagonjwa.

“Benki yenu ya NMB ilianza na mtaji kidogo sana, lakini kadiri siku na miaka inavyozidi kwenda mtaji umekuwa ukikua na sehemu ya mtaji wake asilimia moja kila mwaka tumekuwa tukirudi kwa wananchi na kuwasaidia kama hivi leo mnavyoona tumekuja hapa kwenu”, alisema Mwinula.

Alisema utaratibu huo unalenga kuisaidia jamii yenye hali ya chini kimaisha, ili iweze kuondokana na adha inayopata na hatimaye kusonga mbele kimaendeleo.

Pia Mwinula aliwataka Wananchi wa wilaya ya Nyasa kuweka akiba katika benki hiyo, ikiwemo kuwafungulia akaunti watoto wao ili waweze kujiendeleza kielimu.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Kahindi aliushukuru uongozi wa benki hiyo kuona umuhimu wa kusaidia jamii, hususan katika maeneo ya kutolea huduma za afya na kuwataka waendeleze hilo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Awali benki hiyo ya NMB iliweza kutoa msaada wa Madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano kwa shule ya msingi Komboa iliyopo kata ya Ruanda wilayani Mbinga. 
Sambamba na hilo pia ilitoa msaada wa mashuka 30 na vyandarua 10 katika hospitali ya wilaya hiyo, kwa ajili ya akina mama wajawazito ambao husubiri siku ya kujifungua na kupata matibabu katika hospitali hiyo.



No comments: