Friday, April 25, 2014

HALMASHAURI ZA AGIZWA KUONGEZA VYANZO VYA MAPATO

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Senyi Ngaga, akisisitiza jambo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa ALAT wa mkoa huo, katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy na wa mwisho ni Katibu mkuu wa ALAT wa mkoa wa Ruvuma Mohamed Maje. (Picha na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI za wilaya mkoani Ruvuma zimeagizwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato, ambavyo vitaweza kusaidia kuendesha halmashauri hizo na kuhudumia wananchi badala ya kutegemea ruzuku kutoka kwa wafadhili au serikali kuu.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alipokuwa akifungua mkutano wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT)  ambao ulifanyika juzi katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo.

Ngaga alisema viongozi wa Halmashauri wasipokuwa wabunifu katika kuongeza mapato, hawataweza kwenda mbele na kutimiza malengo ya kuhudumia jamii ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara na miradi ya kilimo.


“Tukijiongezea wigo wa mapato katika maeneo tunayowaongoza wananchi wetu tutaweza kusonga mbele, ni vyema tuzingatie hilo”, alisema Ngaga.
Alisema Halmashauri ikitegemea chanzo kimoja cha mapato kufikia malengo iliyojiwekea itakuwa ni vigumu, na kusababisha kushindwa kutoa huduma husika kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine, Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma alisisitiza pia uboreshaji wa kiwango cha elimu katika shule za msingi na sekondari mkoani humo, ili kuufanya mkoa huo uweze kufikia malengo mazuri ya ufaulu ambayo imejiwekea katika sekta hiyo.

“Natoa wito kwa viongozi wote na wananchi ndani ya mkoa wetu, tushirikiane kuinua taaluma katika shule zetu, tuna kila sababu kuhakikisha tunabadilisha taswira hii ya elimu tuliyonayo sasa na kufikia hali nzuri ya ufaulu”, alisema.

Hata hivyo alieleza kuwa hali ya kiwango cha elimu katika mkoa wa Ruvuma ni mbaya hususan kwa shule za sekondari, hivyo kuna kila sababu kuhakikisha kwamba mkoa huo unajipanga upya katika kutatua tatizo hilo.


No comments: