Tuesday, April 29, 2014

NGAGA AWAPASULIA JIPU MADIWANI MBINGA



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewataka Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo wasiwe watu wa kugeuka geuka, pale wanapoweka misimamo au misingi muhimu ya maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.

Ngaga alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya Madiwani wamekuwa wakishindwa kusimamia makubaliano halali ya vikao husika, badala yake muda mwingi huishia kulumbana na kuzungumzia mambo ambayo hayana tija kwa wananchi.

Kauli hiyo ya Mkuu wa wilaya Mbinga, ilitolewa leo alipokuwa akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo katika kikao cha baraza la madiwani hao kilichoketi leo, kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

“Hii tabia sipendi, tujenge misimamo yetu katika vikao tusiende na manufaa ya mtu mmoja mmoja, tushirikiane katika hili ili mambo yetu yaende vizuri”, alisisitiza.


Aidha Ngaga alilieleza baraza hilo kuwa kuanzia mwaka huu, baadhi ya vijiji 34 vilivyopo wilayani humo serikali itajenga miundombinu ya umeme na kwamba ifikapo mwezi Julai mwakani, kazi hiyo itakuwa imekamilika.

Katika vijiji hivyo 11 vitaunganishwa kwenye mtandao wa gridi ya taifa na 23 vitaingia kwenye mradi wa umeme vijijini, ambapo taratibu husika zimekwisha kamilika na kazi ya ujenzi wa miundombinu  ya umeme wakati wowote kuanzia sasa itaanza kujengwa.

“Ndugu zangu Madiwani hamasisheni wananchi wajenge ushirikiano katika kuona umuhimu wa mradi huu wa umeme, na tutambue kwamba hakuna atakayelipwa fidia yoyote kwenye maeneo ambayo mradi huu unapita, tunachotakiwa tuelimishe wananchi wetu waweze kulielewa hili”, alisema Ngaga.

Pamoja na mambo mengine alikemea kitendo cha Watendaji wa vijiji na kata kutosimamia ipasavyo ujenzi wa miradi ya wananchi, ambapo baadhi yake kama vile majengo ya shule za msingi na sekondari yamejengwa kwa kiwango cha chini jambo ambalo alisema ni ubadhirifu wa fedha za wananchi.

No comments: