Tuesday, April 22, 2014

ALAT RUVUMA YAANZA ZIARA YAKE YA KIKAZI WILAYANI MBINGA

Wajumbe wa Jumuiya ya serikali za mitaa (ALAT) mkoani Ruvuma, wakikagua moja kati ya jengo la kusomea watoto katika shule ya wasichana Kigonsera, iliyopo wilayani Mbinga ambayo inatarajia kuanza kuchukua wanafunzi watakaosoma masomo ya sayansi.

Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho aliyeinama upande wa kushoto, akiangalia moja kati ya meza ambayo itatumika kusomea wanafunzi wa masomo ya sayansi kwenye shule ya sekondari ya wasichana iliyopo katika kata ya Kigonsera wilayani Mbinga.

Baadhi ya Wajumbe wakiangalia mahindi yaliyolimwa na kikundi cha Muungano kilichopo kata ya Kigonsera wilayani humo.

Upande wa kulia aliyevaa suti nyeusi, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Hussein Ngaga akitoa maelezo mafupi kwa Wajumbe wa ALAT wa mkoa huo, juu ya maendeleo ya ujenzi wa Kituo kikuu cha magari ya abiria ambacho kimejengwa Mbinga mjini. Rais Jakaya Kikwete anatarajia kukifungua mapema mwezi Mei mwaka huu. (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAJUMBE wa Jumuiya ya Serikali za mitaa (ALAT) mkoani Ruvuma leo wameanza ziara ya kikazi kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Mbinga mkoani humo.

Aidha licha ya kutembelea miradi hiyo wanatarajia ifikapo Aprili 23 mwaka huu, watafanya kikao chao kujadili maendeleo ya mkoa huo na kuweka mikakati madhubuti ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo, kwa faida ya wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Leo wakiwa katika ziara ya kukagua miradi hiyo wilayani Mbinga, wameweza kujionea shule ya Sekondari ya wasichana (Mbinga girls Secondary school) iliyopo katika kata ya Kigonsera wilayani humo ambayo itaanza kuchukua wanafunzi hivi karibuni.

Shule hiyo ni ya mchepuo wa masomo ya sayansi, inauwezo wa kuchukua wanafunzi 80 watakaosoma hapo na wenye kipaji cha masomo hayo.


Kadhalika Wajumbe hao wa ALAT waliweza kutembelea na kujionea shamba la mahindi kikundi cha Muungano, lililopo katika kijiji cha Kigonsera lenye ekari 80 ambalo wanakikundi husika wameweza kulima mahindi kwa njia bora za kisasa na ujenzi wa barabara kiwango cha lami kilometa moja  Mbinga mjini, ambayo imekamilika.

Baada ya hapo kwa siku ya leo wameweza kuhitimisha ziara yao kwa kushuhudia ujenzi wa Kituo kikuu cha kisasa, magari ya abiria ambacho kimejengwa Mbinga mjini kinachotarajiwa kufanyiwa ufunguzi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete, mapema mwezi Mei mwaka huu.    






No comments: