Saturday, April 12, 2014

MKUU WA MKOA RUVUMA ASEMA HAKUNA ATAKAYEWEZA KUFUTA AGIZO LA SERIKALI

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya waziri Mkuu Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa upande wa kushoto, akiweka sahihi katika kitabu cha wageni alipowasili katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga ambaye ameketi upande wa kulia katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.(Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amesema, hakuna mtu atakayeweza kutengua maamuzi yaliyotolewa na serikali juu ya kuvuliwa madaraka kwa aliyekuwa Ofisa elimu wa shule za sekondari wilayani Mbinga, na Walimu wakuu sita wa shule hizo ambao walihusika katika matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Kauli hiyo ya Mwambungu ilifuatia Mwandishi wa habari hizi alipofanya naye mahojiano juu ya malalamiko yaliyotolewa na Wadau wa elimu wa wilaya hiyo kwa nyakati tofauti wilayani humo, baada ya kuona kumekuwa na njama zinazofanyika chini kwa chini katika jitihada za kutaka kuwarejesha madarakani watuhumiwa hao wanaodaiwa kutafuna fedha hizo.

“Hakuna anayeweza kufuta agizo hili lililotolewa na serikali hatua zitachukuliwa na uamuzi utabaki palepale”, alisema Mwambungu.

Serikali mnamo Februari 7 mwaka huu kupitia Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya waziri Mkuu Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa, alichukua hatua ya kumvua madaraka kwa kumshusha cheo aliyekuwa Ofisa elimu Sekondari Hanji Yusuph Godigodi kwenda kuwa mwalimu wa kawaida akafundishe darasani na wenzake sita ambao ni walimu wakuu wa shule za sekondari, kufuatia kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi na kufanya ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 268 za maendeleo ya elimu ya sekondari wilayani humo.


Wakuu wa shule za sekondari wilayani Mbinga ambao walishushwa madaraka ni William Hyera ambaye ni wa shule ya sekondari Maguu, Clemence Sangana anatoka shule ya sekondari Mkuwani, Method Komba Langilo sekondari, John Tillia Ukilo sekondari, Leonard Juma Luli Sekondari huku akimtaja kwa jina moja mwalimu Konga ambaye yupo sekondari ya Kihangimahuka.

Fedha hizo zinazodaiwa kutafunwa zililenga kufanya kazi ya kununua vitabu kwa shule za sekondari wilayani Mbinga, lakini inashangaza kuona kwamba utekelezaji husika kama serikali ilivyopanga haukufanyika.

Katika fedha hizo shilingi milioni 108 ilibidi zitumike kununua vitabu hivyo, na zinazobakia zifanye shughuli nyingine za maendeleo husika katika shule hizo.

 

No comments: