Wednesday, April 23, 2014

ALAT RUVUMA YALALAMIKIA MWENENDO WA BUNGE MAALUM LA KATIBA

Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho. akisisitiza jambo kwenye kikao chao walichoketi leo Mbinga mjini. Anayefuatia ni mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy na Katibu mkuu wa ALAT mkoani humo Mohamed Maje.

Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

WAJUMBE wa jumuiya ya Serikali za mitaa (ALAT) mkoani Ruvuma, wamesikitishwa na mwenendo wa Bunge maalum la katiba ambalo linaendelea sasa mjini Dodoma, kwa kile walichoeleza kuwa hali hiyo inawakatisha tamaa wananchi.

Walisema asilimia kubwa ya wajumbe wa bunge hilo wamekuwa wakitumia muda mwingi nafasi wanazopewa bungeni, kutetea maslahi yao binafsi na sio kuisaidia jamii ambayo iliwaamini waende huko kutetea na kuwasilisha matatizo ya wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa ALAT wa mkoa huo Oddo Mwisho alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya jumuiya hiyo mbele Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, wakati wa mkutano wao wa siku moja uliofanyika kwenye ukumbi mdogo wa Halmashauri ya wilaya hiyo mkoani humo.

“Mheshimiwa mgeni rasmi pamoja na kukushukuru wewe binafsi kukubali kuwa mgeni wetu, tunakuomba utufikishie salamu zetu kwa serikali hasa kuhusu mwenendo wa Bunge letu la katiba unaoendelea bungeni hivi sasa sisi wanajumuiya hii hatufurahishwi nao”, alisema Mwisho.

Vilevile alieleza kuwa waliopewa dhamana ya kuwakilisha maoni ya wananchi waweke uzalendo mbele kwa kujadiliana kwa hoja badala ya kutumia muda mwingi kulumbana, na matokeo yake kupuuza serikali na kusababisha wananchi wakose imani nayo. 

Alieleza kuwa wao wanaamini wanayoserikali makini ambayo hali hiyo inayo uwezo wa kuidhibiti ili kufikia lengo la kupata katiba ya nchi yenye amani na utulivu na sio kujenga mifarakano isiyo na tija katika jamii. 

Kadhalika alitoa maoni akisema kuna umuhimu kwa bunge hilo la katiba kuingiza masuala ya jumuiya ya tawala za mitaa kwenye katiba inayojadiliwa sasa, kwani hakuna kipengele hata kimoja kinachoelezea juu ya mambo mbalimbali ya jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Ngaga, alipokuwa akifungua mkutano huo wa Jumuiya ya serikali za mitaa alitoa wito kwa wananchi mkoani Ruvuma, kutojiingiza katika ushabiki wa mambo ya katiba badala yake wajikite katika shughuli nyingine za kimaendeleo huku mchakato huo wakiuacha ukiendelea kufanyika huko bungeni.

Pamoja na mambo mengine Ngaga aliwataka Wajumbe wa ALAT mkoani humo wanaporudi katika Halmashauri zao kuhakikisha kwamba wanasimamia ipasavyo mapato na matumizi ya fedha za serikali na kuwa wabunifu wa vyanzo vya mapato badala ya kutegemea ruzuku ya serikali peke yake.

No comments: