Wanabonanza wakiwa katika picha ya pamoja, wakati wakijiandaa kukabidhi baadhi ya vifaa vya kufanyia usafi kwa wafanyabiashara wa soko la wakulima lililopo mjini hapa. |
Tangaza Biashara yako nasi kwa Matangazo ya aina mbalimbali, Mawasiliano zaidi piga simu namba 0762 578960
Wednesday, April 27, 2016
MATUKIO KATIKA PICHA SIKU YA BONANZA LA VIJANA WA MBINGA KUELIMISHA RIKA NA USAFI WA MAZINGIRA MJI WA MBINGA MKOANI RUVUMA
VITENDO VYA USHIRIKINA SHULE YA SEKONDARI NGWILIZI VYADHIBITIWA BAADA YA WAZEE KUKETI PAMOJA DIWANI AELEZEA MIKAKATI YAKE YA KIMAENDELEO
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
VITENDO vya ushirikina ambavyo vilikuwa vikifanyika katika
shule ya sekondari Ngwilizi iliyopo kata ya Kitanda Halmashauri ya mji wa
Mbinga mkoani Ruvuma, vimedhibitiwa baada ya wazee wa kata hiyo kuketi pamoja
na kuzungumzia juu ya kumaliza kero hiyo.
Diwani wa kata hiyo, Zeno Mbunda alisema hayo alipokuwa
akizungumza na mwandishi wetu na kueleza kuwa muafaka huo ulifikiwa baada ya
kukubaliana na wazee hao kwamba, visiendelee kufanyika kwani vimekuwa
vikirudisha nyuma maendeleo ya walimu na wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo
na kata kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga. |
“Wazee wamekwisha kaa vikao na kumaliza tatizo hili, kwa
makubaliano kwamba visiendelee kufanyika tena”, alisema Mbunda.
Awali hivi karibuni katika kikao kilichoketi Aprili 2 mwaka
huu, ilielezwa kuwa walimu na wanafunzi hao hufanyiwa vitendo vya hovyo nyakati
za usiku ambapo huteswa na wakati mwingine wakiwa wamelala, hujikuta wakiwa nje
ya nyumba zao wamevuliwa nguo walizovaa mwilini.
Pamoja na mambo mengine, akizungumzia juu ya mikakati ya kimaendeleo
aliyojiwekea katika kata hiyo Mbunda alisema kuwa wameunda kamati ya kuendeleza
zao la kahawa katika kata hiyo yenye lengo la kuwafanya wananchi wake, waweze
kushiriki kikamilifu katika kuendeleza kilimo cha zao hilo na kukuza uchumi
wao.
Tuesday, April 26, 2016
DED LUSEWA APIGA MARUFUKU VIJANA KUFANYA MAANDAMANO YASIYOKUWA YA LAZIMA
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
MKURUGENZI mtendaji wa Mamlaka ya mji wa Lusewa, wilayani
Namtumbo mkoa wa Ruvuma Astery Mwinuka, amepiga marufuku tabia ya vijana
kufanya maandamano yasiyokuwa ya lazima pindi wanapodai haki zao, badala yake wafuate
sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwemo kutumia Ofisi ya Mamlaka hiyo
katika kutafuta majawabu ya kero zao mbalimbali zinazowakabili.
Mwinuka alitoa onyo hilo, mara baada ya kukabidhiwa
rasmi majengo yatakayotumika kama Ofisi za Mamlaka ya mji wa
Lusewa katika sherehe fupi iliyofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na
wananchi wa kata tatu za Lusewa, Msisima na Magazini ambazo kwa pamoja zimeunda
mamlaka hiyo.
Alisema kuwa tayari serikali imesikiliza kilio chao
kwa kuanzisha mamlaka ya mji huo ambayo itakuwa na dhamana ya kusimamia
shughuli zote za maendeleo, kutatua kero na kukabiliana na changamoto
mbalimbali, hivyo ni vyema wananchi wakawa na utaratibu wa kupeleka kero zao
katika ofisi hizo badala ya kuanzisha migogoro isiyokuwa na tija kwao.
“Tumepata mamlaka ya mji kamili hapa Lusewa, natoa onyo kali
kuanzia sasa hakuna tena maandamano ambayo yatawapotezea muda wenu wa kufanya
kazi kama kuna tatizo tumieni ofisi za mamlaka na sio kukimbilia kwa mkuu
wa wilaya, mtapoteza muda wenu wa kufanya kazi na wengine mtajikuta mkiishia mikononi
mwa vyombo vya dola”, alisema Mwinuka.
BONANZA LA VIJANA MBINGA LASISITIZA MASUALA YA USAFI WA MAZINGIRA PIA LATOA MSAADA WA VIFAA MBALIMBALI KWA WATOTO YATIMA
Baadhi ya wanabonanza la vijana wa Mbinga mkoani Ruvuma, la kuelimisha rika na usafi wa mazingira wakishiriki kuzoa taka katika eneo la soko la wakulima Mbinga mjini. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI waishio katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma, wametakiwa kuzingatia masuala ya usafi kuanzia kwenye mazingira yao
wanayoishi majumbani kwao hadi katika maeneo wanayofanyia kazi au biashara, ili
waweze kuuweka mji huo katika hali ya usafi na kuepukana na magonjwa mbalimbali
ya mlipuko.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga
alipokuwa kwenye maadhimisho ya bonanza la vijana wa Mbinga la kuelimisha rika
na usafi wa mazingira, lililofanyika juzi katika uwanja wa taifa mjini hapa.
Bonaza hilo lilikuwa likienda sambamba na kauli mbiu isemayo;
zuia ngono zembe, mimba za utotoni, madawa ya kulevya na elimu inalipa.
Maadhimisho hayo yalifanyika kwa kuanza kufanya usafi katika
eneo la soko la wakulima lililopo mjini hapa kwa kuwashirikisha wananchi,
watumishi wa serikali na wale wanaotoka kwenye sekta binafsi.
Watoto Yatima wakiwa na Wanabonanza kituo cha Twiga Mbinga. |
Aidha waliweza kuwatembelea watoto yatima ambao wanalelewa
katika kituo cha kulea watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu
kinachofahamika kwa jina la Twiga, kilichopo kata ya Matarawe Mbinga mjini kwa
kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali kama vile sabuni za kuogea na kufulia,
daftari, kalamu, mafuta ya kupikia, sukari, pamoja na sare za shule.
Ngaga alisema kuwa kuna kila sababu katika jamii kuona
umuhimu wa kusaidia watoto hao, ili wasiweze kujiona wakiwa katika hali ya
kutengwa kwa kuwasomesha na hatimaye waweze kutimiza ndoto yao ya kuwa na
maisha bora.
Monday, April 25, 2016
WALIMU WATAKIWA KUWA MABALOZI WAZURI KATIKA KUPINGA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MJUMBE wa Kamati ya utendaji Taifa, Chama Cha Walimu Tanzania
(CWT) mkoani Ruvuma, Jema Mapunda ameipongeza serikali ya awamu ya tano ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa
kutoa elimu msingi bure, ambapo kupitia utekelezaji huo itaweza kuwapa fursa watoto
wa kike kupata elimu hiyo hadi sekondari kwa ufanisi mzuri.
Mapunda alisema hayo juzi, alipokuwa akifungua mafunzo ya
siku moja kwa walimu wanawake viongozi wa CWT mkoani hapa, yaliyofanyika mjini Songea.
Alisema kuwa familia nyingi awali zilikuwa zinasomesha watoto
wao kwa kuwapa kipaumbele watoto wa kiume, huku wakike wakibaki nyumbani kwa
kisingizio cha kukosa ada na michango mbalimbali jambo ambalo hivi sasa limekomeshwa
na Rais Dkt. Magufuli.
NALICHO AWATAKA WATUMISHI KUWAHUDUMIA WANANCHI IPASAVYO MAMLAKA YA MJI WA LUSEWA
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho
amezindua rasmi Mamlaka ya mji wa Lusewa na kumuagiza Mkurugenzi wa
mamlaka pamoja na watumishi waliopelekwa kufanya kazi katika mamlaka hiyo,
kuhamia haraka huko ili waweze kwenda kuwahudumia na kutatua kero
zinazowakabili wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza
na mamia ya wananchi wa kata ya Lusewa, Msisima na Magazini katika
sherehe za uzinduzi wa mamlaka ya mji huo zilizofanyika katika
kijiji cha Lusewa wilayani hapa.
Chande Nalicho. |
Amewaagiza watumishi hao, kwenda kufanya kazi usiku na
mchana kwa kushirikiana na wananchi ili waweze kupata vigezo vya kuwa
halmashuri ya mji badala ya kuendelea kuwa mamlaka ya mji, jambo ambalo
linaweza kuwakosesha baadhi ya vitu muhimu vinavyotolewa na Wizara husika ya Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Alisema kuwa, mamlaka ya mji wa Lusewa ndiyo kwanza
inaanzishwa kwa lengo la serikali kusogeza huduma karibu na wananchi wake hivyo
ni jukumu sasa la watumishi hao kuhakikisha kwamba, wanajitolea muda wao
kufanya kazi na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao
ambao wana mategemeo makubwa baada ya serikali kuanzisha mamlaka hiyo.
MUVI RUVUMA YAWAUNGANISHA WAJASIRIAMALI
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MRADI wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI) mkoani
Ruvuma umeendesha kongamano, lililokutanisha taasisi za kifedha na
wajasiriamali wadogo wadogo kwa lengo la kuwafanya waweze kutambua na kuchagua
ni taasisi gani ya fedha watakayoweza kutumia katika kuendesha shughuli zao za
kilimo, usindikaji na upatikanaji wa masoko ya kuuzia bidhaa zao wanazozalisha.
Jumla ya Wajasiriamali 150 ambao waliwakilisha wenzao 545
waliopo katika mnyororo wa thamani wa zao la mhogo, kutoka wilaya nne za mradi
za Mbinga, Namtumbo, Songea Vijijini, na Nyasa.
Kongamano hilo ambalo lilifanyika juzi katika ukumbi wa chuo
kikuu Huria tawi la Songea, lililenga kuwasaidia wajasiriamali hao waweze
kuchagua ni taasisi gani za fedha wanazoweza kuzitumia katika
shughuli zao za ujasiriamali wanazofanya kila siku na masoko katika zao la mhogo
ambalo sasa lina soko kubwa ndani ya nchi na nje ya nchi.
Thursday, April 21, 2016
WAJUMBE KAMATI YA SIASA WAFUNGA MAKUFULI OFISI ZA CCM NYASA
Na Kassian
Nyandindi,
Nyasa.
WAJUMBE wa Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamefunga kwa makufuli Ofisi za chama hicho
wilayani humo wakishinikiza kuwakataa Katibu wa wilaya hiyo, Greyson Mwengu kutokana
na kudaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha zaidi ya shilingi milioni 50.
Aidha Katibu msaidizi wa CCM wa wilaya hiyo, Mussa Mwevi naye
alikataliwa na kamati hiyo ya siasa kufuatia kutuhumiwa kushiriki kwa namna
moja au nyingine kufanya ubadhirifu huo.
Tukio hilo lilitokea Machi 30 mwaka huu majira ya asubuhi, ambapo
viongozi hao wa Chama cha mapinduzi wilayani humo wanadaiwa kutumia fedha hizo
kinyume na taratibu ambazo zilitakiwa wakawalipe posho viongozi wa matawi,
mabalozi na mawakala kipindi cha uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
TAKUKURU RUVUMA YASEMA HALMASHAURI ZIMESHAMIRI VITENDO VYA RUSHWA
Yustina Chagaka, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani
Ruvuma imesema kwamba, katika mkoa huo watumishi wengi wa serikali wamekuwa
wakijihusisha na vitendo vya kushawishi na kupokea rushwa kutokana na kuwa
watovu wa maadili, katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za kila siku.
Kufuatia hali hiyo, imeelezwa kuwa serikali imeazimia
kupambana na vitendo hivyo na kuwaasa watumishi hao, kuzingatia maadili ya kazi
zao na wananchi washiriki kikamilifu katika kutoa taarifa pale wanapoona au
kusikia kuna harufu ya vitendo vya rushwa.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma, Yustina
Chagaka alipokuwa akitoa taarifa yake ya utendaji kazi kwa waandishi wa habari,
kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.
SERIKALI KUBORESHA MITAMBO YA KURUSHIA MATANGAZO TBC
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
IMEELEZWA kwamba serikali hapa nchini, itahakikisha
inaboresha na kuimarisha mitambo yake ya kurusha matangazo katika mkoa wa
Ruvuma, kupitia redio ya Taifa (TBC) kituo cha Songea ili kuifanya wilaya ya
Nyasa na Namtumbo mkoani humo, ziweze kufikiwa na matangazo mbalimbali
yanayorushwa na kituo hicho kwa ufanisi mzuri.
Kauli hiyo ya serikali inafuatia baada ya wananchi wa mkoa
huo, kulalamika kwa muda mrefu kuwa redio hiyo ya taifa matangazo yake
hayawafikii katika wilaya hizo na badala yake muda mwingi wanapofungua redio
zao, husikia matangazo ya kutoka katika redio zilizopo nchi ya Malawi na
Msumbiji.
Naibu Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Anastazia
Wambura alisema hayo hivi karibuni mjini hapa alipokuwa kwenye kikao maalum akizungumza
na waandishi wa habari, pamoja na baadhi ya watumishi wa serikali mkoani humo.
TASAF SONGEA KUNUFAISHA KAYA MASKINI
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MPANGO wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu katika Halmashauri ya wilaya ya Songea
mkoani Ruvuma, unatarajia kunufaisha kaya 5,016 zilizopo katika wilaya hiyo
ambazo zitapewa ajira za muda na kunufaika na mpango huo, utakaogharimu kiasi
cha shilingi milioni 865,260,000.
Ofisa ushauri na ufuatiliaji wa TASAF katika halmashauri hiyo,
Aniceth Kyaruzi, alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti
hili ofisini kwake mjini hapa.
Kyaruzi alisema kuwa halmashauri ya wilaya ya Songea,
imekwisha anza mchakato wake wa kuibua na kupanga miradi kwa ajili ya kutoa
ajira za muda katika vijiji 37 wilayani humo, ambavyo ni miongoni mwa vijiji 48
vinavyotekeleza mpango huo wa kunusuru kaya maskini.
WAKULIMA WATAKIWA KUNUNUA PEMBEJEO ZINAZOUZWA NA TFA
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKULIMA wa mazao ya chakula na biashara wilayani Mbinga mkoa
wa Ruvuma, wametakiwa kujiunga uanachama na Umoja wa Chama Cha Wakulima Tanzania
(TFA) ili waweze kunufaika na fursa zilizopo, ikiwemo uzalishaji wa mazao yao
kwa ubora unaotakiwa.
Aidha imeelezwa kuwa ndani ya chama hicho, wakulima hao
wataweza kupata elimu juu ya kilimo bora cha kisasa, matumizi sahihi ya pembejeo
na kuingia mikataba na TFA ambayo baadaye itawawezesha kuwatafutia masoko ya
kuuza mazao yao ya chakula na biashara.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipokuwa
akizungumza kwenye maadhimisho ya ufunguzi wa duka la pembejeo za kilimo tawi
la TFA lililopo wilayani humo.
WANANCHI WAITAKA HALMASHAURI KUWAUNGA MKONO
Na Kassian Nyandindi,
Njombe.
WAKAZI wa kijiji cha Mwilamba kata ya Kipengele wilaya ya
Wanging’ombe mkoani Njombe, wameitaka Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya hiyo kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi hao,
juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji vilivyopo kijijini hapo ambavyo ni tegemeo
kubwa kwa mkoa huo.
Aidha wamemuomba Mkuu wa wilaya hiyo, Asumpta Mshama kuacha
kutumia muda mwingi kukaa ofisini badala yake atembelee vyanzo hivyo ambapo walieleza
kuwa serikali ya wilaya, imevitelekeza kwa miaka mingi na kuwaachia wananchi
pekee waendelee kuvitunza.
Kauli hiyo ilitolewa na wakazi hao ambao waliomba majina yao
yasitajwe gazetini, walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari ambao
walitembelea kijijini hapo, kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo.
Saturday, April 16, 2016
WANANCHI WAILALAMIKIA HALMASHAURI YAO
Haya ni madaraja yanayolalamikiwa na Wananchi wa kijiji cha Mwilamba wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe, ambapo ujenzi wake umekuwa ni wa kusuasua. (Picha na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian
Nyandindi,
Njombe.
WANANCHI wa kijiji cha Mwilamba kilichopo katika kata ya
Kipengele wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, wameulalamikia uongozi wa
Halmashauri ya wilaya hiyo kwa kutochukua hatua za haraka kukamilisha ujenzi wa
madaraja mawili yaliyopo katika kijiji hicho, ambayo hivi sasa yanasababisha
washindwe kuendesha shughuli zao za maendeleo.
Aidha wananchi hao walisema kuwa kwa muda mrefu, madaraja
hayo ambayo yalianza kujengwa tangu mwezi Aprili mwaka jana hadi sasa ujenzi
wake unaonekana kusuasua, na hawajui ni lini yatakamilika ili huduma zao za
maendeleo ziweze kutekelezeka bila kuwepo usumbufu wa aina yoyote.
Walifafanua kuwa madaraja hayo, ambayo yapo katika mto
Nang’ano yanaunganisha kijiji cha Mwilamba hadi kwenye barabara kuu ya kutoka
Njombe mjini kwenda wilaya ya Makete.
Baadhi ya wananchi ambao waliomba majina yao yahifadhiwe,
waliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na hali hiyo ya ujenzi wa
madaraja hayo kutokamilika hasa kipindi hiki cha masika, mto huo hufurika maji
na wanashindwa kuvuka kwenda ng’ambo ya pili hasa pale wanapokuwa na wagonjwa
ambao wanapaswa kwenda nao kupata matibabu kwenye kituo cha afya cha Misheni
Kipengele ambacho kipo makao makuu ya kata hiyo.
WAJASIRIAMALI MANISPAA SONGEA WAIANGUKIA SERIKALI
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANAWAKE ambao ni wajasiriamali katika Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kuwaandalia maeneo maalum ya kufanyia
shughuli zao za kila siku ili waweze kujiingizia kipato, badala ya kutumia
maeneo yasiokuwa rasmi ambayo yamekuwa yakiwasababishia adha kubwa wakati
wanapofanya biashara zao.
Baadhi ya wanawake hao walisema hayo hivi karibuni, walipokuwa
wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huku wakieleza kuwa licha ya kujikita
na kutumia zaidi nguvu kubwa katika shughuli zao, changamoto kubwa wanayokabiliana
nayo hivi sasa ni kukosekana kwa mazingira rafiki ya kufanyia shuguli zao badala
yake hulazimika kutumia maeneo ambayo hayajatengwa kisheria jambo ambalo
huwasababishia usumbufu mkubwa, wa kufukuzwa na askari mgambo wa Manispaa hiyo.
Walisema kuwa, jambo hilo linawafanya kushindwa kusonga mbele
kimaendeleo katika maisha yao ya kila siku na hata kushiriki wakati
wa kuchangia shughuli mbalimbali za kijamii.
SHIRIKA LA NSSF RUVUMA LAJIPANGA KUTOA ELIMU KWA WADAU WAKE
Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
SHIRIKA la Taifa
Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani Ruvuma, limejipanga katika kuendelea kutoa elimu
kwa wananchi na watumishi wa serikali kwa kuhamasisha wajiunge na mifuko iliyoanzishwa
na shirika hilo, ili waweze kuepukana na ugumu wa maisha pale wanapofikia hatua
ya kustaafu utumishi wao serikalini.
Kauli hiyo
ilitolewa na Meneja wa shirika hilo mkoani humo, Dominic Mbwette alipokuwa
akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Songea huku akielezea shughuli
mbalimbali, zinazofanywa na shirika hilo.
Mbwette alisema
kuwa kuna baadhi ya wastaafu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu na
wengine hufariki dunia, kutokana na kukosa huduma za msingi katika maisha yao
ya kila siku hivyo ni vyema wajiunge na mfuko huo ili waweze kuondokana na
matatizo hayo yanayowakabili.
DIWANI AJIKUTA AKIINGIA KATIKA KASHFA NZITO NA FEDHA ZA TASAF
Na Steven Augustino,
Tunduru.
DIWANI wa kata ya Tuwemacho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,
Khadija Mohamed amejikuta akiingia katika kashfa nzito baada ya kubainika
alikuwa amejiandikisha miongoni mwa kaya maskini, ambazo zimeingizwa kwenye
mradi wa uhaulishaji fedha unaotekelezwa na Mfuko wa Mendeleo ya Jamii (TASAF)
wilayani humo.
Khadija alibainika kuingizwa kwenye mpango huo, huku
akitambua kwamba anao uwezo wa kujimudu kimaisha, ambapo alibainika kufanya
hivyo baada ya TASAF wilayani hapa kufanya zoezi la kuhakiki majina ya walengwa
wanaostahili kupewa msaada wa fedha hizo ambao ni maskini hawajiwezi.
Sambamba na diwani huyo pia zoezi hilo limemng'oa Kaimu mtendaji
wa kijiji cha Nasya katika kata hiyo, Msamati Omary ambaye naye alijiandikisha
kuwa ni kati ya watu ambao wanastahili kupewa fedha hizo.
Wednesday, April 13, 2016
AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KOSA LA UNYANG'ANYI WA KUTUMIA SILAHA
Na Steven Augustino,
Tunduru.
Yassin Raibu (31) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kazamoyo
wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30
jela baada ya kupatikana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya
hiyo, Gladys Barthy baada ya Mahakama kujiridhisha na kutokuwa na mashaka dhidi
ya ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri, ambao ulipeleka mashahidi saba kwa
ajili ya kuthibitisha kosa hilo lililokuwa likimkabili.
Wakati huo Mahakama hiyo iliwaachilia huru watuhumiwa wengine
wawili waliokuwa wanadaiwa kushirikiana na Raibu katika tukio hilo na kupora
vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 7,175,000 mali ya Said
Khatib Yunusi, mkazi wa kijiji cha Lukumbule wilayani humo.
Saturday, April 9, 2016
TUNDURU WASHUKURU KUPATIWA HUDUMA YA MATIBABU MACHO BURE
Wataalamu wa macho kutoka 'Bilal Muslim Mission Tanzania' wakitoa matibabu ya 'operation' kwa wagonjwa wa macho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WATU 4,292 wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamepatiwa
huduma ya matibabu ya macho kwa lengo la kuboresha afya zao na kuondokana na
matatizo ya macho ambayo yalikuwa yakiwasumbua kwa muda mrefu.
Kati yao, watu 217 sawa na asilimia 5.3 ya wagonjwa wote
waliopatiwa huduma hiyo walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, kansa ya macho,
vikope na majipu yaliyokuwa yakiwasumbua katika macho yao huku wengine wakipewa
miwani kwa wale wote waliobainika kuwa na mahitaji hayo.
Shirika la Bilal Musilm Mission Tanzania, ndilo lililotoa
msaada wa matibabu hayo bure kwa watu hao, ambapo Mratibu wa matibabu hayo Dkt.
Ain Sharif alisema hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya majumuisho ya
utekelezaji wa zoezi hilo lililofanyika katika kambi ya kutolea huduma hiyo, iliyowekwa
shule ya sekondari Frank Weston mjini hapa.
WATOA DAWA MAGONJWA YALIYOSAHAULIKA TUNDURU WAPEWA ONYO
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WATOA dawa kwa ajili ya kinga na tiba ya magonjwa
yaliyosahaulika, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambao wanajiona kwamba
hawaendani na kasi ya utendaji kazi juu ya ugawaji wa dawa hizo, wametakiwa
kujitoa mapema kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yamejitokeza kufuatia uwepo wa taarifa kwa baadhi ya
wagawa dawa katika vijiji vya Nakapanya, Nalasi na vitongoji vyake wilayani
humo ambapo kati yao wametishia kutaka kugomea zoezi hilo wakishinikiza
waongezewe malipo ya ujira wa kufanya kazi hiyo.
Kaimu Katibu tawala wa wilaya ya Tunduru, Augustino Maneno alisema
hayo wakati alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo Chande Nalicho, kwenye
zoezi la kuwaongoza baadhi ya wananchi ambao walijitokeza katika uzinduzi wa
umezaji dawa hizo, uliofanyika hospitali ya wilaya iliyopo mjini hapa.
Magonjwa yaliyosahaulika na yale ambayo hayapewi kipaumbele
(NTD) ni pamoja na magonjwa ya matende, mabusha, ngiri maji na ndiyo ambayo
watu hupewa dawa ili yasiweze kuathiri afya zao.
VITENDO VYA USHIRIKINA VYAWATESA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI NGWILIZI
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa vitendo vya ushirikina ambavyo vinaendelea
kufanyika katika shule ya sekondari Ngwilizi iliyopo kata ya Kitanda Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya walimu na
wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo.
Diwani wa kata hiyo, Zeno Mbunda amekemea hali hiyo na
kueleza kuwa walimu na wanafunzi hao hufanyiwa vitendo vya hovyo nyakati za
usiku ambapo huteswa na wakati mwingine wakiwa wamelala, hujikuta wakiwa nje ya
nyumba zao wamevuliwa nguo walizovaa mwilini.
Senyi Ngaga Mkuu wa wilaya ya Mbinga. |
Mbunda alisema hayo alipokuwa kwenye kikao cha kujadili
maendeleo ya kata ya Kitanda, kilichoshirikisha Wenyeviti wa vijiji na wazee
ambacho kilifanyika juzi katika kata hiyo huku akiongeza kuwa hali hiyo
inasababisha hata kwa watumishi wengine wa serikali waliopo huko, wanaishi kwa
hofu wakiogopa mambo hayo ya ushirikina.
“Haya mambo wazee wenzangu hayafai inatupasa tuwe imara
tubadilike, watoto nyakati za usiku pale shuleni hawalali wanateswa, masuala
kama haya wanaoyafanya mnawafahamu, inabidi tuwaite tukae nao na kukemea hali
hii kwa sababu wanaleta hofu kwa wengine na kushindwa kuishi kwa amani”,
alisema Mbunda.
KITUO CHA AFYA MSINDO CHAKABILIWA NA TATIZO LA UKOSEFU WA MAJI
Na Julius Konala,
Namtumbo.
KITUO cha afya Msindo, kilichopo katika Halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo mkoani Ruvuma, kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
ukosefu wa maji na umeme jambo ambalo linakwamisha utendaji kazi kwa watumishi
waliopo katika kituo hicho.
Jimmy Runje ambaye ni Mganga mkuu wa kituo hicho alieleza
kuwa wanapohitaji huduma ya maji, hulazimika kuyafuata umbali mrefu na
kuwafanya kuwa katika wakati mgumu hasa pale wanapofikia hatua ya kufua mashuka
ya kulalia wagonjwa.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na mganga mkuu huyo alipokuwa
akizungumza na mwandishi wetu, ambaye alitembelea kituo hicho kwa ajili ya
kujionea changamoto mbalimbali.
Thursday, April 7, 2016
DOKTA MAGUFULI ASHIRIKI SHUGHULI ZA KUMBUKUMBU MAUAJI YA KIMBARI KIGALI NCHINI RWANDA
Rais
wa Rwanda Paul Kagame akimpokea Rais Magufuli katika viwanja vya Gishozi kabla
ya kwenda kuweka mashada ya maua, kwenye makaburi ya watu waliouwawa katika
mauaji ya Kimbari.
Rais
wa Rwanda Paul Kagame akiwa na Rais Magufuli pamoja na Mama Janeth Magufuli,
Janeth Kagame wakielekea kwenye makaburi ya halaiki katika makumbusho ya mauaji
ya Kimbari, Gishozi Kigali nchini Rwanda.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakisali
mbele ya makaburi ya watu waliouwawa katika Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda
mwaka 1994. Kulia ni Rais wa Rwanda Paul Kagame pamoja na Mkewe Janeth Kagame
na mtoto wake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakisali
mbele ya makaburi ya watu waliouwawa katika Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda
mwaka 1994. Kulia ni Rais wa Rwanda Paul Kagame pamoja na Mkewe Janeth Kagame
na mtoto wake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame wakiwasha mwenge
wa matumaini kuashiria kutotokea tena kwa mauaji ya Kimbari nchini Rwanda.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth Magufuli wakiangalia kwa
uchungu mafuvu ya watu waliopoteza maisha katika mauaji hayo ya kimbari.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame, mama
Janeth Magufuli, Mama Janeth Kagame wakisikiliza historia ya jinsi mauaji ya
kimbari yalivyotokea katika eneo la kumbukumbu ya mauji hayo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame, mama
Janeth Magufuli, Mama Janeth Kagame waiwa wamesimama kutoa heshima kwa watu
waliofariki katika mauaji hayo ya kimbari.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashiriki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiwa miongoni mwa wageni
mbalimbali waliofika kwenye kumbukumbu hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia picha za watoto waliouwawa kinyama katika
eneo la Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbaria
Gishozi Kigali nchini Rwanda.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli akisaini Kitabu katika Jengo la makumbusho ya mauaji
ya Kimbari Gishozi Kigali nchini Rwanda.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea kitabu chenye maelezo mbalimbali
kuhusu mauaji hayo ya kimbari. (Picha na IKULU)
WAKAGUZI ELIMU NAMTUMBO WATAKIWA KUONGEZA KASI UTEKELEZAJI MAJUKUMU YA KAZI ZA KILA SIKU
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
WAKAGUZI wa elimu katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo
mkoani Ruvuma, wametakiwa kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yao
ya kazi ikiwemo kutembelea shule za msingi na sekondari mara kwa mara na
kuwachukulia hatua kali za kisheria, walimu wazembe ambao wanasababisha
wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao ikiwa ni mkakati wa
kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho
alipokuwa akizungumza na wakaguzi wa idara ya elimu ofisini kwake mjini hapa, ambapo
alikemea tabia ya wakaguzi kutumia muda mwingi kukaa ofisini na kuwaacha walimu
peke yao wakitumia muda mwingi wa kazi kufanya shughuli zao binafsi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba, hata tatizo la kushuka
kwa ufaulu katika wilaya ya Namtumbo linachangiwa na idara ya
ukaguzi kwa kushindwa kutembelea shule hizo kwa kuwafuatilia
utendaji kazi wa walimu hao.
MILONJI LUSEWA WATAKIWA KUPELEKA WATOTO WAO SHULE
Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Milonji, kata
ya Lusewa wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameaswa kupeleka kwa wingi watoto
wao shule ili waweze kupata elimu, ambayo itawasaidia kutoka katika hali ya
umaskini unaowakabili kwenye familia zao.
Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho alitoa rai hiyo juzi alipokuwa
akizungumza na wazazi na walezi pamoja na wananchi wa
kijiji hicho, katika mkutano wa hadhara wenye lengo la kutafuta
majawabu ya kukabiliana na changamoto zilizopo za watu kutotaka
kupeleka watoto wao shule, alipokuwa kwenye ziara ya siku mbili katika
kata ya Lusewa wilayani humo.
Chande Nalicho. |
Alisema kuwa, baadhi ya wazazi wamekuwa hawatendi haki kwa watoto
wao kwa kuwapa mahitaji ya msingi ikiwemo suala la kuwapatia elimu, jambo
ambalo ni sawa na ukatili mkubwa unaofanywa na wazazi kwa watoto
wao.
Alisisitiza kuwa kila mzazi anaowajibu wa kuhakikisha watoto alionao
watakapofikisha umri wa kwenda shule, ni lazima wawe wameripoti shule
ili wapate elimu ambayo ni urithi endelevu katika maisha yao ya kila
siku.
Mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo alifafanua kuwa hadi kufikia
mwishoni mwa mwezi uliopita, tayari shule ya msingi
Milonji imekwisha andikisha watoto 107 na imekuwa shule ya 8 ambayo
inaongoza kwa kuitikia wito wa Rais Dkt. John Magufuli ya elimu bure.
JAMII YATAKIWA KUJIUNGA NA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
USHAURI umetolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani
Ruvuma kwamba, Halmashauri za wilaya, mji na manispaa mkoani humo
kuanza utaratibu wa kutunga sheria maalum, itakayowabana watu wote wasiotaka
kujiunga na mfuko wa afya ya jamii na bima ya afya.
Abdiel Mkaro, ambaye ni Meneja wa NHIF Mkoani humo ametoa
ushauri huo alipokuwa akizungumza na gazeti hili juu ya mwamko mdogo wa
wananchi kujiunga na mfuko huo, kwa ajili ya kupata huduma bora za matibabu
pindi wanapougua.
Halmashauri hizo amezitaka kuhakikisha kwamba zinaongeza dawa
katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zake ili wanachama waliojiunga na
mfuko huo waweze kupata huduma ipasavyo pale wanapokwenda kupata
huduma kutokana na maradhi yanayowasumbua, ambapo baadhi ya maeneo wanachama
wamekuwa wakikosa dawa jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa wananchi
wengine kuogopa kujiunga na mpango huo.
Wednesday, April 6, 2016
MHANDISI ASHINDWA KUTOLEA MAELEZO JUU YA UJENZI WA MADARAJA
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MHANDISI mkaguzi wa barabara na majengo Halmashauri ya mji wa
Mbinga mkoani Ruvuma, Jordan Kapinga amejikuta akiwa katika wakati mgumu
kufuatia Diwani wa kata ya Kitanda katika halmashauri hiyo, Zeno Mbunda kumtaka
atolee maelezo juu ya kwa nini ujenzi wa madaraja na barabara umejengwa kwa
kiwango cha chini ndani ya kata hiyo.
Hali hiyo ilifuatia baada ya Diwani huyo kuibua hoja hiyo,
katika kikao maalum cha Wenyeviti na wazee wa vijiji vya kata hiyo kilichoketi
kwenye ofisi za makao makuu ya kata ya Kitanda Aprili 2 mwaka huu, kwa lengo la
kujadili maendeleo ya kata hiyo na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wake.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. |
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunda alisema kuwa ujenzi wa
barabara na madaraja matatu ambao umefanywa katika kata hiyo haujashirikisha
wananchi na mkandarasi husika aliyepewa kazi hiyo hakuripoti kwa uongozi wa
kata hiyo jambo ambalo linawafanya wajenge shaka.
Kampuni ya Ndapa Interprises Corporation Company Limited
kutoka Dar es Salaam, alisema kuwa ndiyo iliyopewa kazi hiyo ambapo ujenzi wa
barabara na madaraja hayo umefanyika kwa kiwango cha chini.
Sunday, April 3, 2016
MKUU WA WILAYA SONGEA AWATAKA WANANCHI WAKE KUSHIRIKI KWENYE ZOEZI LA UMEZAJI DAWA
Na Julius Konala,
Songea.
MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Benson Mpesya
amewaongoza baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Songea katika zoezi la
umezaji dawa kwa ajili ya kinga na tiba ya magonjwa yaliyosahaulika
na yale ambayo hayapewi kipaumbele (NTD) mjini hapa, ikiwemo ugonjwa wa matende.
Mpesya aliwaongoza wananchi hao katika uzinduzi uliofanyika
kwenye Zahanati ya gereza la Mahabusu mjini Songea, kwa kumeza dawa hizo za
kinga na tiba ya magonjwa ya usubi, mabusha, ngilimaji, trakoma, kichocho na
minyoo ya tumbo.
Akiwahutubia wananchi, wanafunzi wa shule ya msingi Majimaji,
walimu, askari magereza na watumishi wengine wa serikali waliojitokeza katika uzinduzi
huo, aliwataka kuondoa hofu na dhana potofu ya kwamba dawa hizo kwamba zina
madhara na kuwa na busha sio heshima katika jamii, bali ni matatizo makubwa.
Mkuu huyo wa wilaya aliwahimiza wananchi wengine, kujitokeza
kwa wingi katika kushiriki zoezi hilo linaloendelea mjini hapa pindi wataalamu
watakapokuwa wanazungukia maeneo mbalimbali, ikiwemo majumbani, shuleni na
katika vyuo.
Friday, April 1, 2016
WANANCHI TUNDURU WAPATIWA HUDUMA YA MATIBABU MACHO BURE
Na Steven Augustino,
Shirika la Bilal Musilm Mission, ndilo lililotoa huduma hiyo ambapo Dkt. Ain Sharif ambaye ni mratibu wa huduma hiyo alisema kuwa ilikuwa ikitolewa hivi karibuni katika shule ya sekondari, Frank Weston iliyopo mjini hapa.
Tunduru.
ZAIDI ya watu 5,000 waishio wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamenufaika
na huduma ya matibabu ya macho iliyotolewa wilayani humo kwa lengo la kuboresha
afya zao, kutokana na wengi wao kusumbuliwa na matatizo mbalimbali ya magonjwa
ya macho.
Shirika la Bilal Musilm Mission, ndilo lililotoa huduma hiyo ambapo Dkt. Ain Sharif ambaye ni mratibu wa huduma hiyo alisema kuwa ilikuwa ikitolewa hivi karibuni katika shule ya sekondari, Frank Weston iliyopo mjini hapa.
Sharif alisema kuwa jumla ya madaktari 12 wakiwemo madaktari
bingwa watano wa huduma za macho walishiriki katika zoezi hilo, ambalo lilidumu
kwa muda wa siku nne.
KAMPUNI YA USAFIRISHAJI ABIRIA KUPUNGUZA ADHA YA USAFIRI RUVUMA
Na Julius Konala,
Songea.
KAMPUNI ya
usafirishaji abiria mikoani inayofahamika kwa jina maarufu la, Ilyana Company
Limited ya jijini Dar es salaam, imepanua huduma zake kwa kufungua ofisi zake
katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na kufanya idadi ya makampuni ya
usafirishaji mjini hapa, kuwa matatu.
Akizungumza na
gazeti hili ofisini kwake mjini Songea, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo,
Khalfan Kigwenembe alisema kuwa lengo la kufungua ofisi hiyo ni kwa ajili ya kuwasaidia
wananchi wa Manispaa ya Songea na mkoa kwa ujumla kusafiri kwa bei nafuu ambayo
imepangwa na serikali.
Kigwenembe ambaye
pia ni Diwani wa kata ya Namtumbo mjini, wilayani Namtumbo mkoani hapa, kupitia
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema kuwa mabasi ya kampuni hiyo
yatafanya safari zake kuanzia Songea, Mbinga, Namtumbo hadi Dar es Salaam.
JESHI LA POLISI LAMSAKA ASKARI WAKE ALIYETOROKA BAADA YA KUGHUSHI VYETI VYA MASOMO
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamsaka askari wake
wa kikosi cha kutuliza na kuzuia ghasia (FFU) mkoani humo mwenye namba F 5425
PC Emmanuel Nyagoli (35) kwa kosa la kutoroka jeshini, baada ya kukabiliwa na
tuhuma ya kugushi vyeti vya masomo wakati alipokuwa akijiunga na jeshi hilo
mwaka 2003.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa
Polisi mkoani humo Zubery Mwombeji alisema kuwa askari huyo alitoroka tangu Machi
16 mwaka huu, ilipobainika kwamba ametenda kosa hilo.
Mwombeji alisema kuwa PC Emmanuel, alikuwa ni askari wa
kikosi cha kutuliza na kuzuia ghasia na kwamba alipogundulika kuwa ana tatizo
hilo, ndipo alitoroka na kutokomea kusikojulikana.
WAKULIMA NYASA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA ZAO LA KOKOA
Na Mwandishi wetu,
Nyasa.
WAKULIMA wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamehimizwa kulipokea
zao jipya la kibiashara la Kokoa, kwa lengo la kuongeza kipato chao na kuimarisha
uchumi wa wilaya hiyo kwa ujumla.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkuu wa wilaya Nyasa, Margaret Malenga
alipokuwa akizindua kilimo cha zao hilo wilayani humo, ambao ulifanyika
katika kijiji cha Songambele kata ya Kihagara.
Malenga alisema kuwa endapo watazingatia kilimo cha zao hilo,
wananchi hao wataweza kuongeza vipato vyao na kuwafanya kuachana na tabia ya kutegemea
shughuli za uvuvi pekee.
Subscribe to:
Posts (Atom)