Wednesday, January 15, 2014

CHAMA CHA WALIMU MBINGA KWA CHAFUKA, NAIBU KATIBU MKUU TAIFA APOKELEWA KWA MABANGO

Baadhi ya Wanachama wa CWT wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali ambayo yanawashutumu Katibu wao wa mkoa huo Zebedayo Mwasandungila na wa wilaya hiyo Samwel Mhaiki, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kwa hasira alikataa kuyasoma na kuwaambia Wajumbe wa mkutano huo twendeni kwanza ndani kwenye ukumbi tukafanye mkutano.



Bado Wajumbe wa mkutano huo wakiwa ndani ya ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa ambako mkutano huo ulikuwa ukifanyika, wakiwa na hasira na kuendelea kushika mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali ambao ulikuwa ukiwashutumu baadhi ya viongozi wao wa mkoa na wilaya ya Mbinga .

Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania, Ezekiah Oluoch, akihutubia katika ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, mara baada ya Wanachama wa chama hicho kutuliza jazba zao. Upande wa kulia ni Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo na kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga. (Picha zote na Kassian Nyandindi) 



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Ezekiah Oluoch amejikuta akiwa katika wakati mgumu, baada ya kupokelewa na wanachama wa chama hicho wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa malalamiko ya hapa na pale na mabango yaliyobeba ujumbe wa aina mbalimbali ambayo yalikuwa yakiwashutumu Katibu wa CWT wa mkoa huo na Wilaya hiyo.

Waliokuwa wakishutumiwa ni Zebedayo Mwasandungila ambaye ni Katibu wa CWT mkoa wa Ruvuma na Samwel Mhaiki, Katibu wa chama hicho wilayani Mbinga ambao wanalalamikiwa kutengeneza makundi ndani ya chama.

Vilevile Mhaiki alikuwa akinyoshewa kidole kwamba yeye na kamati yake ya chama wilayani humo, wameshindwa kukiongoza chama na badala yake makato wanayokatawa wanachama ya asilimia 15 katika mishahara yao hawarejeshewi katika matawi yao, hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kubaki na viongozi hao na kuwataka wajiuzuru mara moja.

Walisema wamekwisha mpatia Bw. Mhaiki notisi ya siku 30 kwa lengo la kusudio la kumfikisha Mahakamani ili haki zao ziweze kupatikana.

“Tumekwisha mwona mwanasheria kwa lengo la kusudio la kumfikisha Mahakamani ndugu Samwel Mhaiki, na sasa tumempatia notisi ya siku 30 atuambie fedha zetu za makato ya kila mwezi zipo wapi”, walisikika wakisema kwa sauti.


Aidha Wanachama hao walikuwa wakiendelea kupaza sauti wakisema Mwasandungila amekuwa akiwatumia meseji za matusi pale wanapodai haki zao za msingi na kuwatishia usalama wa maisha yao.

Kwa upande wa Mhaiki walieleza kuwa ameshindwa kuwaongoza na anatumia madaraka yake pasipo kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa katika chama, hivyo hawana sababu ya kuendelea kuwa naye hapa wilayani hivyo aondoke naye.

Wakati Naibu Katibu Mkuu Oluoch akisikiliza kilio cha Wanachama hao kwenye ukumbi wa jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, huku wakimtaka asome ujumbe wa mabango waliyoyabeba ghafla alionekana kuwa mkali na kukataa kuyasoma na kusema twendeni tuingie ukumbini tuzungumze siwezi kuyasoma haya mabango yenu.

Kwa ujumla mabango yaliyokuwa yamebebwa na wanachama hao yalikuwa yamebeba ujumbe uliokuwa ukisomeka kwamba; karibuni Mbinga kwenye ufisadi, Mwenyekiti wa CWT ajiuzulu Mbinga sio msaada kwetu, tunahitaji Katibu atakaye kiimarisha chama na sio mbabaishaji, tumechoka na meseji za kashfa na matusi za Mwasandungila na Mhaiki hatukutaki wilaya ya Mbinga wewe ni mzigo.

Baada ya Wajumbe kuingia ukumbini hali ilikuwa sio shwari ambapo wanachama hao waliendelea kumweleza Naibu Katibu Mkuu wa CWT Taifa Bw. Oluoch kwamba, wamekwisha wasilisha barua zao za kujitoa uanachama na sasa wamefikia jumla yao 547 ambao wanatoka katika maeneo mbalimbali wilayani Mbinga na huku wakiongeza kuwa wengine bado wanaendelea kujiandikisha kwa ajili ya kujitoa.

“Mheshimiwa Naibu Katibu mkuu, tumeandika barua za kujitoa uanachama na kusitisha makato mara moja katika mishahara yetu yasiendelee kufanyika, tunachodai ni madai yetu ambayo tunakidai chama toka mwaka 2011 tumechoka na hawa watu na sasa ondoka nao”, alisema Edmund Hyera mwalimu wa shule ya msingi Juhudi kata ya Kigonsera.

Akisoma taarifa kwa niaba ya Wanachama wenzake mbele ya Naibu Katibu Mkuu Taifa, Mwalimu Stella Mhagama kutoka shule ya msingi Mtua kata ya Mpepai alisema wamechoshwa na vitendo vinavyofanywa na kamati tendaji ya CWT wilayani Mbinga kwa kutengeneza migogoro kati ya walimu na mwajiri wao, kwa kuandika mabarua ya kuchafuana na kuyapeleka kwa viongozi wa ngazi ya juu.

Pia Mhagama alisema, wamechoshwa na kamati hiyo kwa kile alichoeleza kuwa imekuwa ikitumia lugha za kashfa kwa Wanachama pale wanapohitaji maelekezo muhimu ya kichama kutoka kwao kwa nyakati tofauti.

Alieleza kuwa licha ya Wanachama kuandika barua za malalamiko na kuzipeleka makao makuu ya CWT Taifa, hakuna utekelezaji uliofanyika hivyo wao wamechoshwa na tabia inayofanywa na viongozi wa chama hicho hapa wilayani na kusema, hawaoni sababu ya kuendelea kuwa wanachama badala yake watajitoa.

Pamoja na mambo mengine akijibu hoja za malalamiko ya Wanachama hao Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Taifa, Ezekiah Oluoch alikiri ofisi yake kupokea malalamiko hayo akisema……….“ndugu zangu wanachama kwanza kabisa mimi naomba niwaombee radhi hawa viongozi waliowakosea kwa haya yote yaliyojitokeza hapa kwenu wilayani”.

Oluoch alisema ni kweli Katibu wa mkoa na wa wilaya hiyo wanamakosa na ndio waliosababisha kuwepo kwa changamoto hizo hivyo wamwachie yeye anakwenda kuyafanyia kazi kwa kukaa na viongozi wenzake wa makao makuu ya chama.

“Dawa nzuri kwa haya yote yaliyojitokeza kwa mtu muungwana ni kuomba radhi kwa matatizo haya niliyoyaona, kwa niaba yao naomba niwaombee radhi na hawa walimu 547 msijitoe kwanza acheni hiyo njooni tukijenge chama”, alisema Oluoch.

Alifafanua kuwa kinachotakiwa viongozi wa CWT mkoani humo wametakiwa kuwa makini na utekelezaji wa majukumu yao ya kazi na sio wakati wote kuchochea vurugu ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya chama.

Hata hivyo alisema hivi sasa chama hicho kimeweka utaratibu wa kuzunguka nchi nzima na kutoa semina kwa walimu, ili waweze kutambua haki zao za msingi katika chama jambo ambalo litasaidia kuondoa migogoro isiyo kuwa ya lazima.

No comments: