Thursday, January 2, 2014

MLINZI AUAWA NA MAJAMBAZI KWA KUKATWA KOROMEO


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MLINZI wa kituo cha kuuza mafuta GAPCO kilichopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, amekutwa akiwa ameuawa kikatili na watu wasiojulikana kwa kukatwa koromeo na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili imeelezwa kuwa aliyeuawa ni Kelvin Mapunda(52) mkazi wa mjini hapa, ambapo mwili wake ulikutwa ukiwa umetelekezwa karibu na eneo la kituo hicho cha mafuta.

Mwandishi wa habari hizi alipofika katika eneo la tukio hilo, alikuta umati mkubwa wa watu ukiwa umezunguka mwili wa marehemu huyo huku wakionekana kuchukizwa na kitendo hicho cha kinyama.


Kamanda wa polisi wa mkoa huo Deusdedith Nsimeki alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Desemba 31 mwaka huu majira ya saa 12 asubuhi.

Alisema watu hao ambao wanadaiwa kuwa ni majambazi sugu wamefanya mauaji hayo na kupora kasiki ambalo ndani yake lilikuwa na fedha shilingi milioni 8.4 ikiwa ni mauzo ya siku iliyopita.

Hata hivyo Nsimeki amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kujenga ushirikiano na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa mbalimbali za kiuhalifu ili hatua madhubuti ziweze kuchukuliwa dhidi ya watu au kundi lenye dhamira mbaya ya kuvuruga amani katika jamii.

No comments: