Wednesday, January 29, 2014

DOKTA KAMANI AFUNGUKA AWATAKA WAFANYAKAZI WASIOENDANA NA KASI YAKE WAJIONDOE MAPEMA




Na Mwandishi wetu,


WAZIRI  wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dokta Titus Kamani, amesema ili kwenda na kasi ya maboresho ya wizara hiyo, inahitajika dhana ya uwajibikaji na uwazi sambamba na kujitolea kwa nguvu zote katika kufanya kazi.

Kamani, aliyasema hayo juzi katika mkutano wa kwanza uliowakutanisha wafanyakazi wote wa wizara hiyo, wakiwemo wastaafu wa mwaka jana katika ofisi ya wizara hiyo ilizopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Alisema kama kuna mtu ambaye ni kikwazo katika kukwamisha shughuli za wizara, ni bora akawapisha mapema na kwamba kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa kuifanya kazi kwa uwazi na akaitaka wizara kufanya kazi na vyombo vya habari kwani ndio njia pekee ya kuwafanya watanzania wajue wizara inafanya nini.

“Wewe upo ofisini, halafu unaogopa ogopa vyombo vya habari, kwani unatatizo gani kuweni wazi mambo yenu yawe hadharani watanzania wa Mbeya wayajue, Rufiji mpaka Pemba, hakuna kuficha ficha jambo katika wizara yangu.” alisistiza Dokta Kamani.

Alisema wizara ya maendeleo ya mifugo na uvuvi ndio moyo wa taifa kwani huwajumuisha watanzania wengi wenye maisha ya kawaida, lakini amesikitishwa kwa jinsi ambavyo wizara hiyo imekuwa ikichukuliwa na baadhi ya watu kama ni wizara yenye migogoro na kuleta hasara maeneo mengine.


“N'gombe hawa wamekua wakiingia kwenye hifadhi, wanapigwa risasi, wanaaribu mashamba ya watu na kuleta njaa kwa wananchi, ng'ombe hawa wamekuwa wakisema wanaleta uharibifu wa mazingira kwa wananchi kwa sababu ya kuhamahama, kama ng’ombe hawa ungepatikana utaratibu mzuri wa kuwatunza na kuwahifadhi basi, taifa hili lingeingiza kipato kikubwa ikiwemo kuuza nyama hadi nje ya nchi, maziwa na kuboresha afya za watanzania” alisema Dokta Kamani.

Dokta Kamani, amesema anafahamu wizara yake ina changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo bajeti kuwa ndogo, lakini kwa kutumia taaluma yake pamoja na ushirikiano wa wafanyakazi wote wa wizara hiyo, anaamini itakuwa ni wizara yenye neema kwa watanzania, yenye kueneza ajira na kipato kwa sababu hakuna jambo lisilowezekana kama kila mmoja atafanya kazi kwa dhamira moja.

Akizungumzia juu ya ranchi za taifa, waziri Kamani amesema ana nia ya dhati ya kuona ranchi za taifa zinafufuka na kutengeneza uchumi imara wa taifa, kuzalisha ngombe wenye ubora ambao watatoa mazao ya mifugo yatakayoliingizia taifa hili kipato kikubwa.

Akizungumzia sekta ya uvuvi Waziri Kamani alisema sekta hiyo ni tabu tupu alisema leo tunaambiwa kuna uvuvi haramu, nyavu zisizokidhi viwango na huku wavuvi wakiendelea kuwa masikini, katika nchi yenye bahari, maziwa na mito mikubwa kila kona, ameuliza ni kweli wanahitaji bajeti kubwa ya kushughulika na mambo hayo?.

“Tunahitaji utashi wa kuwasadia wavuvi wetu, kwa kutoa elimu na kufanya mazungumzo nao ya mara kwa mara, kuwatembelea maeneo yao ya kazi na kubaini matatizo yao kisha kuyafanyia kazi”, alibainisha.

Kuhusu zao la kuku Waziri Kamani alisema hivi sasa kuna tatizo la mayai feki na chanjo feki, alihoji ni kweli kwamba wafanyakazi wa wizara hiyo haiwajui wahusika au kuna baadhi ya watumishi ndio miradi yao? ambapo aliagiza wizara kubaini wanaofanya biashara hiyo feki ambayo inaleta madhara hasa wakazi wa mjini ambao ni watumiaji wakubwa wa bidhaa hizo.

No comments: