Thursday, January 2, 2014

UWT MBINGA YAWATAKA AKINA MAMA KUEPUKANA NA MAKUNDI YA ANASA

Wanachama wa UWT wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi zawadi zao walipokwenda kuwataka hali akina mama wenzao ambao wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa.


Upande wa kushoto aliyevaa shati la kijani ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Pendo Ndumbaro akifurahia jambo baada ya kushika mtoto mchanga ambaye alizaliwa usiku wa kuamkia mwaka mpya (2014) alipokuwa ametembelea jana wodi ya akina mama katika hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa kwa lengo la kuwataka hali, na wanaoshuhudia ni baadhi ya akina mama ambao wamelazwa katika hospitali hiyo. (Picha zote na Kassian Nyandindi).



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
WANAWAKE wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa makini katika kuendesha maisha yao kwa kujishughulisha na kilimo, biashara na kujiunga na vyama vya akiba na mikopo ili waweze kuepukana na kujiingiza kwenye anasa ambazo zinachangia maambukizi ya virusi vya ukimwi.
 
Sambamba na hilo wameshauriwa kushirikiana na kuchukua hatua katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku kwa kufanya kazi kwa bidii.

Rai hiyo ilitolewa  jana na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Mbinga Pendo Ndumbaro, alipokuwa akizungumza na akina mama waliolazwa katika hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa ambao aliwatembelea kwa lengo la kuwataka hali na kuwapa zawadi mbalimbali.

Pia Mwenyekiti huyo alikuwa ameambatana na wanachama wenzake wa umoja huo ambao walishiriki kwa pamoja kwenda kuwaona wagonjwa hao waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo.


“Ndugu zangu Mungu akitusaidia baada ya kupona ni wakati sasa wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii,   wanawake wengi tumekuwa tukijiingiza kwenye anasa kutokana na kutokuwa na ajira kama njia ya kujipatia kipato, yatupasa tubadilike tuachane na mambo haya”, alisema.  
 
Alisema huu ni wakati wa wanawake kujikwamua kiuchumi ikiwemo pia kwa kujiunga kwenye SACCOS ambazo zitawasaidia kuwajengea uwezo kwa kupata mikopo ya kuanzisha na kuimarisha miradi yao.
 
Kadhalika alieleza kuwa wanawake wanapaswa kujiendeleza kielimu na kupambana na maisha kwa kufanya shughuli za kimaendeleo, badala ya kushindana kwa mambo yasiyo na msingi.

Aliwataka wanawake kutambua kuwa wao ni kiungo muhimu katika jamii hivyo ni vyema serikali, ikawawekea vipaumbele mbalimbali ili waweze kujikwamua kimaisha kwa kuwa asilimia kubwa wao ndio walezi wa familia.

No comments: