Thursday, January 2, 2014

WAKIMBIA FAMILIA ZAO WAKIHOFIA KUKAMATWA NA POLISI


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BAADHI ya Wanaume wa kijiji cha Mbangamao kati, kata ya Mbangamao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamezikimbia familia zao wakihofia kukamatwa na polisi baada ya kuvamia nyumba ya Mratibu elimu wa kata hiyo Florence Kowelo, na kumjeruhi kwa kumpiga nondo kichwani.

Watu hao wanadaiwa kufanya kitendo hicho na kutishia usalama wa Watumishi wengine wa serikali, katika kata hiyo baada ya kuwatuhumu wamekuwa na tabia ya kufanya mapenzi na wake zao.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Desemba 27 mwaka huu na kwamba vibaka hao ambao wanatamba kijijini hapo kwa jina la M 23, kuwa wameapa kupambana na Watumishi wote waliopo katika kata ya Mbangamao.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisa mtendaji wa kata hiyo Elnea Mwanyekule alisema Wanaume hao ambao majina yao hakutaka kuyataja kwa sababu za kiusalama, wamezikimbia familia zao na kwenda kusikojulikana baada ya kutokea vurugu hizo.  

“Hivi sasa amani na utulivu katika eneo hili imekuwa ni tatizo, watu Wafanyakazi tunaishi kwa wasiwasi kutokana na kundi hili ambalo limekuwa likitamba muda mwingi kuwa litaendelea kupambana na watumishi waliopo hapa”, alisema.

Kuhusu madai ya kwamba Watumishi wa kiume waliopo katika kata hiyo wanatabia ya kufanya mapenzi na wake za watu, Mwanyekule alikanusha na kusema kuwa kauli hizo si za kweli bali kundi hilo litakuwa na sababu zingine ambazo yeye hazifahamu.

Diwani wa kata ya Mbangamao Christantus Mbunda, naye alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alithibitisha kuwepo kwa vurugu hizo na kusema kuwa tayari hatua za kulisaka kundi hilo zinafanyika, kutokana na vibaka hao kuendelea kuleta vitisho vya kutaka kumuua mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mbangamao Mathayo Kivinga.

Mbunda alisema hatua za awali zimechukuliwa kwa kumuhamisha Mratibu elimu wa kata hiyo ambaye amejeruhiwa na mwalimu huyo wa shule ya msingi, ili kuweza kunusuru maisha yao wakati taratibu zingine za kisheria zinaendelea kuchukua mkondo wake.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsimeki amesema jitihada za kuwasaka vibaka hao zinaendelea kufanyika, na kuongeza kuwa taratibu husika zitakapokamilika watafikishwa Mahakamani.

No comments: