Wednesday, January 29, 2014

GUNINITA AMRUSHIA KOMBORA NAPE


Na Mwandishi wetu,
Dar es Salaam.

KITENDO cha Katibu mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Nape Nnauye cha kupinga uteuzi wa Mawaziri uliofanywa na Mwenyekiti wa chama hicho ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwendelezo wa tabia zake za ukosefu wa nidhamu kwa viongozi wake.

Hayo yamo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa hivi karibuni, ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es salaam, John Guninita  amesema Nape ni mkiukwaji wa maadili, asiyeheshimu wakubwa ambao wamemteua kushika nafasi hiyo.

Alisema ni kiongozi ambaye anatakiwa kufanya kazi kwa  kuzingatia mipaka yake hivyo ni vema akafahamu kuwa madaraka ya kuteua Baraza la mawaziri ni kazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na sio vinginevyo.

Guninita alisema hata kama ingetokea Rais akashauriwa na washauri zaidi ya mia moja, bado uamuzi wake unapaswa kuheshimiwa na hakuna mtu anayeweza kuingilia au kubeza.


Alisema kitendo cha Nape kutoa maneno ya dhihaka ni mwendelezo wa tabia zake za kuropoka na kujitwalia madaraka makubwa zaidi ya mwenyekiti au katibu wa CCM Taifa.

"Yote yaliyotamkwa na Nape kwenye mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni ni mawazo yake binafsi na sio ya chama kwani hakuna kikao chochote kilichokaa na kumtuma akaongee mambo haya”, alisema.

Guninita alimtaka Nape kuacha kuwaita wenzake kuwa ni mizigo, badala yake ajitazame kwanza yeye mwenyewe kama ni msafi ndani ya chama hicho au la kutokana na kile alichoeleza kuwa amekuwa akikiyumbisha chama kutokana na kauli zake.

No comments: