Monday, December 23, 2013

UJENZI WA BARABARA KIWANGO CHA LAMI SONGEA HADI MBINGA UTATA MTUPU

Na Kassian Nyandindi,
Songea.
 
UJENZI wa barabara kiwango cha lami kuanzia eneo la Likuyufusi pacha ya Peramiho wilaya ya Songea hadi Mbinga, umeanza kuzua malalamiko kutokana na barabara hiyo kuanza kuwekwa viraka kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali.
 
Barabara hiyo ambayo ni ya kilometa 78 inagharimu kiasi cha shilingi bilioni 79.8 na kutekelezwa chini ya mradi mkuu wa changamoto za milenia Tanzania (MCAT).
 
Fedha za ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni mwa dola 698 za Kimarekani zilizotolewa nyakati za mwisho katika utawala wa Rais mstaafu George Bush, ikiwa ni sehemu ya msaada kwa ajili ya kujenga miradi mbalimbali ya kimaendeleo hapa nchini.
 
Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti wakati mwandishi wa habari hizi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Songea na Mbinga, ambapo walisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona ujenzi wa barabara hiyo kabla haijakabidhiwa rasmi imeanza kuwekwa viraka baadhi ya maeneo.
 
“Kwa kweli hatukutarajia kama leo hii barabara inajengwa kwa kiwango cha lami halafu kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali inabomoka na kuwekwa viraka, maana viongozi walituhakikishia barabara yetu itajengwa vizuri na kwa kiwango bora”, walisema.
 
Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited kutoka nchi ya China , ndiyo imekabidhiwa kazi ya ujenzi wa kiwango cha lami  na kwamba ujenzi wake hadi kukamilika umechukua zaidi ya miezi 27.
 
Huu ni mradi mkubwa wa pili hapa mkoani Ruvuma, wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambao umetanguliwa na mradi mwingine wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Songea hadi Namtumbo ikiwa ni utekelezaji wa maendeleo ukanda wa Mtwara.
 
Utekelezaji huo ambao umepewa jina maarufu “Mtwara Corridor” umelenga kuunganisha barabara kwa kiwango cha lami kutoka bandari ya Mtwara, bahari ya Hindi hadi bandari ya Mbamba bay ziwa Nyasa wilayani  Mbinga.
 
Hata hivyo Mwandishi wa habari hizi alipomfuata Meneja wa Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma Abraham Kissimbo ofisini kwake, ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo alimtuma muhudumu wake wa ofisi na kumweleza kuwa hana nafasi ya kuweza kuzungumza na mwandishi wa habari hizi.
 
 

No comments: