Thursday, December 5, 2013

KUKOSEKANA KWA SHULE MAALUM YA WALEMAVU WILAYANI MBINGA KUNASABABISHA WALEMAVU KUKOSA HAKI ZAO ZA MSINGI

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga (upande wa kulia) akizungumza na wananchi na watu wenye ulemavu katika kijiji cha Luhagara kata ya Litumbandyosi wilayani humo, katika maadhimisho ya sherehe za siku ya walemavu.

Kutoka kushoto Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Allanus Ngahy, katikati ni Diwani wa kata ya Litumbandyosi James Yaparama na upande wa kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo Ngaga, akiweka sahihi katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa maadhimisho ya sherehe hizo kijiji cha Luhagara. (Picha zote na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa shule maalum kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kunasababisha watu hao kukosa haki zao za msingi za kupata elimu, ambayo ingelifanya kundi hilo, kuweza kuondokana na maadui wawili ujinga na umasikini.

Kutokana na ukosefu huo baadhi yao kutoka katika familia zenye uwezo mkubwa hulazimika kwenda kusoma mikoa mingine ambayo ipo mbali kwa kutumia gharama kubwa, hivyo serikali imeombwa kunusuru hali hiyo kwa kujenga shule ya watu wenye ulemavu wilayani humo.

Hayo yalisemwa na Katibu mkuu wa Chama Cha Walemavu (CHAWATA) wilayani Mbinga Kassian Nyandindi, wakati alipokuwa akisoma risala ya watu wenye ulemavu hivi karibuni mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, katika siku ya maadhimisho ya sherehe za watu hao zilizofanyika kijiji cha Luhagara kata ya Litumbandyosi wilayani humo.

Wakati akisoma taarifa hiyo alisema bado kundi hilo linakabiliwa na tatizo la miundo mbinu ya majengo mbalimbali kutokuwa rafiki kwao na gharama kubwa ya viungo bandia kuwa bei ghali na kufikia hatua wengi wao hushindwa kuvinunua.

Vilevile watu wenye ulemavu wilayani humo wamelalamikia kukosa uwakilishi kuanzia ngazi ya mtaa, vitongoji mpaka kwenye vikao vya Madiwani (Full Council) ili uwakilishi huo uweze kutetea haki zao za msingi.


Kwa upande wake akijibu risala hiyo Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, alisema matatizo hayo ameyapokea hivyo kwa yale ambayo yapo ndani ya uwezo wa wilaya hiyo yatafanyiwa kazi, na mengine ambayo yapo nje ya uwezo yatafikishwa ngazi ya juu serikalini kwa ajili ya utekelezaji zaidi.

Pia Ngaga aliwataka Wazazi na walezi wilayani humo, kuendelea kuwathamini na kuwajali watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mahitaji au huduma muhimu ili baadaye waweze kujitegemea.

“Ndugu zangu walemavu ni Watanzania wenzetu hivyo tunalojukumu la kuwa nao pamoja kwa kuwashirikisha katika shughuli za kimaendeleo na sio kuwatenga au kuwaficha ndani, mzazi atakayebainika kufanya hivi serikali itamchukulia hatua za kisheria”, alisema Ngaga.

Kadhalika aliongeza kuwa ni muhimu wapelekwe shule kwa kile alichoeleza kuwa wengi wao, wanaouwezo mkubwa wa kufanya vizuri endapo wanapewa nafasi au fursa mbalimbali.  


No comments: