Wednesday, December 18, 2013

MKUU WA MKOA WA RUVUMA ALIA NA WAKUGURUGENZI WA HALMASHAURI KUWAPA KAZI WAKANDARASI WAZEMBE

Na Muhidin Amri,

Ruvuma.

SERIKALI mkoani Ruvuma imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri  za wilaya katika mkoa huo, kutowapa tena zabuni Wakandarasi ambao ni wababaishaji, wazembe na wenye rekodi mbaya katika utendaji wa kazi zao, ili wasiweze kuisababishia serikali hasara ya kuingia gharama nyingine upya ya ujenzi wa miradi ya Wananchi.

Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha siku moja cha Wajumbe wa jumuiya ya serikali za mitaa(ALAT) kilichofanyika mjini Namtumbo mkoani humo, ambapo alitumia nafasi hiyo kupiga marufuku wakandarasi wasiokuwa na sifa kuomba na kufanya kazi katika mkoa wa Ruvuma kwani wamekuwa wakiurudisha nyuma maendeleo ya taifa letu kwa ujumla.

Mwambungu amesikitishwa na usimamizi mbovu wa fedha zinazotolewa na serikali wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali, ambapo imebainika kuwa wakandarasi wengi wamekuwa na tabia ya wizi kwa kuingia mikataba hewa na halmashauri husika na wakishapata fedha hukimbia bila kukamilisha kazi walizoomba kufanya, tatizo ambalo alidai kuwa linachangiwa kwa kiasi fulani na baadhi ya watumishi hasa wakuu wa idara wasiokuwa waaminifu.

Alisema ni kosa kumpa kazi Mkandarasi mwenye rekodi mbaya huku akiwaonya Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri  juu ya tabia ya kuwa na urafiki wa jirani na wakandarasi hao kwa kile alichoeleza kuwa kinatokana na tamaa ya fedha huku akisisitiza ni vema  kutoa kipaumbele kwa wakandarasi waaminifu  na wenye sifa ambao wanatimiza majukumu yao ya kazi kwa viwango vinavyotakiwa.


“Serikali haiwezi kuwavumilia wakurugenzi, wenyeviti na hata wakandarasi wa aina hii ambao kila kukicha  kazi yenu ni kutafuta kuiba na kufanya mambo kwa maslahi yenu, tabia hii kwa kweli hatuwezi kufika mbali kwani  mnachangia sana kurudisha nyuma maendeleo katika mkoa wetu”, alisema Mwambungu.

Alibainisha kuwa sio kosa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na Mwenyekiti wakwe kuwa na urafiki na wakandarasi,  lakini uhusiano wao   usiwe chanzo cha kushindwa kukemea au kumchukulia hatua  iwapo  mtu  aliyempa kazi atashindwa kutimiza majukumu yake.   
Aidha Mkuu huyo wa mkoa ametaka kasi ya ukusanyaji mapato ya ndani katika  Halmashauri kuongezeka kwani   hivi sasa hakuna hata halmashauri moja katika mkoa huo inayokusanya kufikia asilimia 4  kati ya asilimia 100 hivyo kutegemea fedha kutoka serikali kuu  kwa ajili ya miradi na shughuli nyingine za maendeleo jambo ambalo ni vigumu kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Kadhalika Mwambungu amezitaka Halmashauri mkoani Ruvuma, kuimarisha na kusimamia vizuri vyanzo vilivyopo vya mapato ili viweze kuleta tija kama ilivyokusudiwa na serikali, kwa lengo la kutaka kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

No comments: