Sunday, December 1, 2013

MBINGA WATAKIWA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
VIONGOZI kwa kushirikiana na Wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuhakikisha kwamba wanakabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, na sio kusubiri nguvu au misaada kutoka nje jambo ambalo ni hatari kwa kizazi cha sasa na kijacho.
 
Rai hiyo ilitolewa na Wananchi wa wilaya hiyo walipokuwa wakitoa maoni yao kwenye mdahalo uliohusu athari za mabadiliko ya tabia nchi, ambao ulikuwa ukiendeshwa na shirika lisilo la kiserikali (MBINGONET) lililopo wilayani humo, uliofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.
 
Walisema kuwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, viongozi kwa kushirikiana na jamii lazima wabuni ufumbuzi wao wenyewe na sio kungojea misaada kutoka nje, wakati wilaya hiyo na taifa kwa ujumla linazidi kuangamia siku hadi siku.
 
Mkazi mmoja wa Mbinga mjini Godfrey Ngonyani alieleza kuwa imefika wakati sasa, elimu itolewe katika jamii juu ya kunusuru hali hiyo isiweze kuendelea na Viongozi hapa nchini wanapaswa kushikilia msimamo wa kuhakikisha kuwa athari hizo tunakabiliana nalo, na kama haitafanyika hivyo ni wazi kuwa tunatengeneza mazingira mabaya ambayo ni hatari hapo baadaye.
 
“Halmashauri ziwe na mpango endelevu juu ya namna ya kuboresha mazingira ambayo hayatakuwa chanzo cha uharibifu wa hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kuwa na mazingira yaliyokuwa safi na kupanda miti katika maeneo mbalimbali hususani kwenye vyanzo vya maji”, alisema Ngonyani.
 
Awali kwa upande wake, Mgeni rasmi Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga Idd Mponda ambaye alifungua Mdahalo huo alisema halmashauri zimejifunza mambo mengi ikiwemo namna ya kuendeleza halmashauri kwa kuzingatia mfumo sahihi, wa utunzaji wa miji na mazingira kwa ujumla.
 
Mponda alisema wameweza kupata maelezo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu, kutoka katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na mazingira.
 
Hata hivyo alisisitiza kuwa wilaya ya Mbinga ni kama wilaya zingine zote zilizopo hapa nchini, hivyo itahakikisha inakabiliana na tatizo hilo ili kuweza kupata ufumbuzi wa kina, kuepusha madhara yanayoweza kupatikana kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
 
 

No comments: