Tuesday, December 17, 2013

KADA WA CHAMA CHA MAPINDUZI AFARIKI DUNIA KWA KUJINYONGA


















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KADA mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Lulambo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kujinyonga katika msitu uliopo jirani na kitongoji hicho.

Tukio hilo ambalo limetokea hivi karibuni, imethibitishwa kuwa Kada huyo ambaye ni Gisberth Haulle (45) alikuwa Mwenyekiti wa tawi la Ngamanga kupitia tiketi ya CCM ambalo lipo katika kitongoji hicho.  

Kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Lulambo, Gisberth Ndimbo alisema chanzo cha tukio hilo inadaiwa kuwa marehemu huyo alifikia uamuzi wa kujinyonga kutokana na ugomvi ambao ulidumu kwa muda mrefu katika familia yao.


Chanzo cha ugomvi huo kinaelezwa kuwa walikuwa wakigombania mashamba yeye na ndugu zake baada ya kutaka kuuza sehemu mojawapo ya shamba, ili aweze kupata fedha za kumpeleka mtoto wake shule.

Kufuatia hali hiyo ndugu walikataa na kwamba, ndipo Haulle alichukua maamuzi magumu ya kwenda kujinyonga na hatimaye kupoteza maisha yake.

Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, limethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kufafanua kuwa uchunguzi bado unaendelea ambapo baadhi ya ndugu wanaendelea kuhojiwa.

No comments: