Wednesday, December 18, 2013

AURIC AIR YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE MKOANI RUVUMA

















Na Mwandishi wetu,
Songea.

WAKAZI wa mkoa wa Ruvuma wameombwa  kuunga mkono juhudi mbalimbali za wawekezaji wanaokwenda kuwekeza katika mkoa huo, badala ya kubeza kwani hali hiyo inaweza kuwakatisha tamaa wawekezaji hao na hatari ya kubaki watazamaji  na  mabingwa  wa kusifia maendeleo yaliyopo kwenye mikoa mingine.

Wito huo umetolewa mjini Songea na mfanyabiashara   Abbas Hemani wakati akizungumza na Mwandishi wetu, kuhusu fursa nyingi za uwekezaji zilizopo katika mkoa wa Ruvuma na kuongeza kuwa iwapo wakazi wa mkoa huo hawataunga mkono juhudi hizo basi mkoa huo,   utabaki na umasikini licha ya kuwepo kwa fursa na rasilimali nyingi.

Abbas ambaye  ni wakala wa shirika la ndege la AURIC AIR ambalo ndege zake hufanya safari kati ya Dar es slaam na Songea mkoani humo, amewaomba wakazi wa mkoa huo hususani wafanyabiahara kutumia usafiri wa ndege za kampu8ni hiyo, ili kumuunga mkono katika jitihada zake  za kutaka mkoa wa Ruvuma unakuwa miongoni mwa mikoa  yenye usafiri wa uhakika  na kusaidia kuleta maendeleo.

Alisema lengo la kuanzisha usafiri huo wa ndege ni  kuisaidia serikali katika kuboresha baadhi ya huduma ambazo yenyewe ilishajitoa, hivyo kutoa nafasi kwa wananchi wenye uwezo  waweze kuwekeza katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwahudumia  wananchi.


Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa maeneo ambayo usafiri wa kufika makao makuu ya nchi jijini Dar es slaam  kwa viongozi, wafanyabiashara na wananchi wengine ulikuwa mgumu kutokana na umbali uliopo ambapo ni zaidi ya kilometa 1000 lakini tangu kuanza kwa safari za ndege hizo, imekuwa rahisi  kwao kufika maeneo mengine kwa ajili ya shughuli mbalimbali ambazo  siku za nyuma ilikuwa ni vigumu.

Aliongeza kuwa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 25 hutumia  muda wa masaa mawili kutoka Dar es slaam hadi Songea, na sasa tayari katika miezi mitatu mfululizo imekwishasafirisha zaidi ya watu 400 na matarajio yake kuwa itaongeza idadi, iwapo tu kutajitokeza mahitaji makubwa kutoka kwa wananchi.
 
Kwa upande wake  Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amepongeza jitihada za wakala huyo na  kampuni ya AURIC AIR kwa kukubali kuanzisha usafiri wa ndege mkoani Ruvuma, ukizingatia kwamba ni muda mrefu walikuwa na mahitaji ya usafiri  huo lakini hakuna kampuni yoyote iliyokubali kuleta ndege zake licha ya jitihada za mara kwa mara kwa makampuni ya ndege kuyaomba kufanya  hivyo.  

Naye mfanyabiashara  maarufu wa mjini Songea Mohamed Hussen, alieleza kuwa hivi sasa wanajivunia kuwepo kwa usafiri huo katika kuboresha biashara zao, na hata ikitokea mteja anahitaji bidhaa ambazo zipo mbali inakuwa rahisi kuagiza au kufuatilia tofauti na siku za nyuma kabla ya kuanzishwa kwa usafiri huo wa anga.


No comments: