Sunday, December 22, 2013

MAHAKAMA KUTOA MAAMUZI JUU YA MAUZO MBAO ZILIZOKAMATWA KATIKA OPARESHENI TOKOMEZA UJANGILI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MAHAKAMA ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, imepanga kutoa maamuzi ya kuuza au kutouzwa kwa mbao 8,328 zenye thamani ya shilingi milioni 291.4 ambazo zilikamatwa kupitia “Oparesheni tokomeza ujangili”, iliyofanyika hivi karibuni kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu.

Hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo Ernest Mgongolo alisema hayo wakati alipokuwa akijibu, maombi yaliyotolewa na Mawakili waliokuwa wakiwakilisha upande wa serikali katika kesi tano zinazowakabili watuhumiwa saba ambao walinaswa wakati wa oparesheni hiyo wakiwa na na mbao hizo kinyume cha sheria.

Watuhumiwa hao ni wakazi wa Jijini Dar es Salaam na Mtwara  ambapo awali wakitoa maombi, Wanasheri  wa serikali  Mwahija Sembeni na Francis Aloyce waliiomba Mahakama kwa mamlaka iliyonayo kutumia kifungu cha sheria namba 352 kifungu kidogo (2) kinacho ambacho huruhusu kutoa kibali cha kuuzwa kwa kidhibiti chochote au mali ambayo ipo mbele ya mahakama na yenye kuweza kuharibika.



Kwa nyakati tofauti Wanasheia hao walisema kuwa maombi hayo wameyatoa baada ya kubaini kuwa baadhi ya mbao hizo zimeanza kuharibika kutokana na kuoza na eneo zilipokuwa zikitunzwa haikuwa salama, na imekuwa kero kwa watumishi wa idara ya Maliasili wilayani Tunduru.

Aidha wanasheria hao waliwatoa mashaka Watuhumiwa hao kuwa kuuzwa kwa mbao hizo hawatakuwa wamepoteza haki zao, kwa madai kwamba baada ya kuuzwa mbao hizo fedha hizo zitahifadhiwa katika akaunti maalum na kwamba fedha hazitatolewa na kukabidhiwa kwa mtu atakayeibuka na ushindi baada ya mahakama kufikia maamuzi yake ya mwisho.

Wakijibu hoja hizo kwa nyakati tofauti Wanasheria wa upande wa utetezi waliojitambulisha kwa jina moja moja la Ogunde na Kerukelwa walipingana na maombi ya upande wa Jamuhuri, kuwa endapo mbao hizo zitauzwa wao watakosa ushahidi wakati wa kuwasilisha utetezi wa wateja wao kwa madai kuwa miongoni wa vitu wanavyotaka kuvitumia kupitia mbao hizo ni alama za mihuri iliyogongwa katika mbao ili kuthibitisha kama ni mali ya hao watuhumiwa au la.

Watuhumiwa wanaokabioliwa na kesi hiyo ni Amiri Simbeni na Francis Aloyce walikamatwa na mbao 2154, Nehemia Kiondo aliyenaswa na mbao 427, Sofia Nhama kutoka alinaswa akiwa na mbao 1965.

Wengine waliokamatwa na vibali bandia ni Steven Buhanza akiwa na mbao 2317, Athuman Mussa na Zablon Kambaye.

Awali ilidaiwa Mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao wote walikutwa wakiwa na mbao hizo, huku wakiwa na vibali vya kughushi ambavyo vilidaiwa kutolewa na nchi Jirani ya Msumbiji kinyume cha sheria.

Washtakiwa wote walikana mashitaka hayo na wapo nje kwa dhamana hadi Januari 27 mwakani, ambapo mahakama hiyo itatoa maamuzi juu ya mashtaka wanayokabiliana nayo.

No comments: