Sunday, December 22, 2013

TAMCU TUNDURU WALIA NA TAKWIMU ZA KOROSHO



Na Steven Augustino,

Tunduru.

CHAMA kikuu cha ushirika Wakulima wa korosho wilaya ya Tunduru (TAMCU) mkoani Ruvuma, kimefanikiwa kukusanya tani  554 ambazo ni kidogo, kati ya tani 9115 zilizokadiriwa kuzalishwa katika msimu wa mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Katibu mkuu wa chama hicho wilayani humo, Imani Kalembo akiwemo na Mwenyekiti wake Mahamudu Katomondo mbele ya waandishi wa habari, waliokuwa wakifanya mahojiano nao mjini hapa juu ya maendeleo ya uzalishaji wa zao hilo.

Viongozi hao walifafanua kwamba wamepata wakati mgumu kukusanya takwimu hizo za uzalishaji, kwa kile walichoeleza kuwa kutokana na wilaya hiyo kuwa na utaratibu mbovu uliotumika kununulia zao hilo katika msimu wa mwaka huu.

"Takwimu tulizowapeni ni zile ambazo tu zimetokana na manunuzi yaliyofanywa na TAMCU kupitia vyama 18 vya ushirika vya wakulima ambavyo vipo katika tarafa za Lukumbule, Namasakata, Nalasi, Matemanga, Mlingoti Nakapanya na Namtumbo ambako chama kilipeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa Korosho", alisema Kalembo.



Kadhalika viongozi hao walipongeza maamuzi ya serikali kwa kuruhusu mfumo wa soko huria, kutumika katika msimu huu kutokana na wilaya ya Tunduru wakulima wake kukosa wanunuzi katika misimu miwili iliyopita hali ambayo ilisababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakulima.

Walisema kupitia utaratibu huo msimu wa mwaka huu jumla ya makampuni 11 yalichuana kununua korosho wilayani humo, ambayo ni Export Trading company Limited, Prayosa, Kulaathool company Limited, Shareeji Impex Limited, Said Mohamed Said pamoja na  Olam Tanzania Limited.

Makampuni mengine yaliyoomba  kununua korosho  kupitia mfumo wa soko huria ni China Pesticide Tanzania Limited, Amina Seti, Saweya Impex Tanzania Limited, Alpha Choice Limited, Sunrise Commodities pamoja na Chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa korosho wilayani Tunduru (TAMCU).

Pamoja na mambo mengine makampuni hayo yaliwekewa utaratibu wa kuhakikisha kwamba yanafuata sheria na taratibu husika za manunuzi zilizowekwa, ikiwemo kununua zao hilo kutoka kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika pamoja na kulipa ushuru na kodi zote zilizoainishwa katika mikataba yao huku wakitakiwa kutonunua kwa bei isiyopungua shilingi 1100.

No comments: