Tuesday, December 17, 2013

TUNDURU WAWEKA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA NJAA, SHERIA KUUNDWA KUWABANA WAZEMBE



Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa kila kaya inakuwa na chakula cha kutosha wilayani humo ili kuweza kuepukana na baa la njaa ambalo linaweza kutokea hapo baadaye.

Mikakati hiyo inaenda sambamba kwa kuanza kuwapeleka Mahakamani  watu wote, ambao hawatakuwa na mashamba ya kuzalisha mazao ya chakula katika msimu wa mvua wa mwaka huu na kuendelea.

Chande Nalicho ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo, ndiye aliyetangaza msimamo huo wa serikali na kuitaka jamii ya wanatunduru kuhakikisha suala hilo linatekelezwa mara moja.

Kadhalika serikali itafanya mzunguko kwa kupita kutoa elimu kwa wananchi wote wilayani Tunduru, na kwamba kesi za wavivu zichukuliwe hatua kwa walengwa wanaoshinda vijiweni ikiwemo kufungwa.

Msimamo huo ulitangazwa na mkuu huyo wa wilaya, wakati alipokuwa akizungumza katika mdahalo wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza njaa duniani uliofanyika katika ukumbi wa Sky way, uliopo mjini hapa.

Mdahalo huo ulihusisha viongozi wa madhehebu ya dini na kuungwa mkono juu ya tamko hilo, ikiwemo kuundwa kwa sheria ndogo ambayo itafanya utekelezaji huo uweze kuleta ufanisi.

Kwa ujumla wilaya ya Tunduru wakazi wake asilimia 84 wanategemea shughuli za kilimo, na katika mipango yake ya kawaida wilaya hiyo imejiwekea mikakati ya kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara katika msimu wa mwaka 2013 hadi 2014.

 Akitoa ufafanuzi katika mdahalo huo Askofu wa jimbo la Tunduru – Masasi, Castory Msemwa alizitaka mamlaka na jamii kwa ujumla wanajenga ushirikiano katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa ipasavyo na kuzaa matunda.

Alisema kutokana na  ukosefu wa elimu, vitendea kazi, pembejeo za uhakika na utawanyaji miundombinu yake ambao umekuwa usioaminika vimekuwa ni kati ya vikwazo vikubwa katika jamii kukosa chachu ya maendeleo katika sekta ya kilimo.

Askofu Msemwa pia aliwataka wananchi kuungana na shirika la Caritas lililopo jimboni humo,  katika kukabiliana na upungufu wa chakula ambao unaweza ukajitokeza hapo baadaye.

No comments: