Wednesday, December 11, 2013

VYAMA VYA KUWEKA NA KUKOPA VYATAKIWA KUTOA TAARIFA SAHIHI KWA WANACHAMA WAKE



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

VIONGOZI wa Chama cha kuweka na kukopa (SACCOS) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kujenga ukweli na uwazi katika utendaji wa kazi zao za chama, na sio kutoa taarifa zisizo sahihi kwa wanachama ambazo baadaye zinaweza kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima.

Aidha wametakiwa kutuoa ushirikiano wa kutosha kwa Mamlaka husika ambayo inasimamia vyama vya ushirika, kufanya ukaguzi na kutoa hali halisi ya mwenendo wa chama kwa wanachama, ili waweze kuwa na uhakika wa usalama wa mali zao.

Rai hiyo ilitolewa na Ofisa elimu Msingi wilaya ya Mbinga, Mathias Mkali alipokuwa mgeni rasmi kwenye mkutano mkuu wa chama cha kuweka na kukopa cha Mbinga Kurugenzi SACCOS, uliofanyika kwenye ukumbi wa Jimbo la Mbinga uliopo mjini hapa.

Vilevile aliwashauri wanachama wa umoja huo, wahakikishe kuwa wanarejesha mikopo waliyokopa kwa wakati ili chama kiweze kusonga mbele.

“Napenda niwashauri, tujenge tabia ya kurejesha mikopo tunayokopa kwa wakati uliopangwa na tukifanya hivyo chama hiki kitakuwa na mzunguko mzuri kifedha, pia ili tuweze kufanikiwa jambo hili elimu ya ushirika itolewe kwa wanachama”, alisema Mkali.


Awali kwa upande wake Meneja Mkuu wa Mbinga Kurugenzi Saccos, Raymond Mhagama alisema chama hicho kwa kipindi cha mwaka huu kuanzia mwezi Januari hadi sasa, kimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 190,503,000.

Pia Mhagama alifafanua kuwa katika kipindi hicho wameweza kurudisha akiba, amana na hisa zenye thamani ya shilingi milioni 110.3 kwa wanachama waliokoma uanachama wao.

No comments: