![]() |
Mtambo ukiendelea na uchimbaji wa Makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka, huko katika kijiji cha Ntunduaro kata Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
HATUA iliyochukuliwa na Serikali kupiga
mabomu kwa ajili ya kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kwa amani katika
kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda mkoani Ruvuma, Mbunge wa jimbo la Mbinga
Gaudence Kayombo, ameshusha lawama nzito na kusema hajafurahishwa na kitendo
hicho.
Gaudence Kayombo
amesema, nguvu iliyotumika ni kubwa na hapakuwa na sababu kwa serikali kufanya
hivyo, kutokana na wananchi wa kijiji hicho madai yao wanayoyadai ni ya msingi
na muda mrefu sasa, umepita hawajatekelezewa.
Mbunge huyo alisema
hayo alipokuwa akihojiwa na Mwandishi wa habari hizi juu ya wananchi hao
wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu, wakidai fidia zao katika eneo ambalo
waliondolewa kwa ajili ya kupisha shughuli za mgodi wa Ngaka, ambapo huchimbwa
makaa ya mawe.
”Kule imetumika nguvu
kubwa ya polisi kupiga mabomu wale wananchi, hapakuwa na sababu badala yake
serikali itoke mbele na ieleze hawa wanaodai fidia zao lini watalipwa”, alisema
Kayombo.
Alisema kuwa kuna
baadhi yao wengine hawajalipwa kabisa na wananchi karibu 400 ambao awali
walilipwa fidia zao, ilionekana fedha walizolipwa ni kidogo hivyo nao walipewa
ahadi ya kuongezewa malipo mengine, jambo ambalo hadi leo hii halijatekelezwa.
Kayombo alisisitiza
akisema ni vyema serikali itimize wajibu wake, kwa kuelimisha wananchi na sio
kutumia nguvu kubwa kwa kuwapiga mabomu ambayo yanaathiri jamii.