Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amesema kwamba ni aibu kuona au kuendelea kusikia katika zahanati na vituo vya
kutolea huduma za afya vilivyopo wilayani humo, kwamba fedha zipo za kununulia
dawa lakini wagonjwa wanalalamika hakuna dawa.
Nshenye alisema kuwa hivi karibuni alitembelea katika
baadhi ya vituo hivyo wilayani hapa na kukuta malalamiko hayo ambapo kufuatia
hali hiyo ameagiza kuwa endapo itaendelea sasa utafika wakati wa wahusika
kuwajibishwa pale atakapoona kuna tatizo kama hilo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo wakati alipokuwa
akihutubia katika kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya Mbinga
mkoani humo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Alisema kuwa panapotokea hakuna dawa katika vituo hivyo
vya afya sio tatizo la serikali ni tatizo na uzembe wa watendaji wa kada hiyo,
kwani fedha za kununulia dawa hizo zinakuwepo ila kunakuwa na uchelewaji wa
kuziagiza kutoka Bohari Kuu ya Madawa (MSD) iliyopo hapa nchini.
“Nimefanya ziara ya kutembelea vituo hivi, lakini vingi
vilikuwa havina dawa kwa hiyo nirudie kusema panapotokea hakuna dawa sio tatizo
la serikali ni tatizo la watendaji wetu tutaendelea kushughulikia hili na
kushughulika nao”, alisisitiza Nshenye.
Kadhalika Nshenye aliwataka viongozi ndani ya wilaya
hiyo wajipange sasa katika jukumu la kuongeza ujenzi wa vituo vya afya ili
kuweza kusogeza huduma karibu na wananchi.
Hata hivyo alisisitiza kuwa katika ujenzi huo
wahakikishe kwamba kwa mujibu wa sera ya afya ndani ya vituo hivyo wanajenga
chumba cha upasuaji na wodi za kulaza wagonjwa hasa ikilenga kuweza kutoa
huduma karibu na akina mama wajawazito ambao wanaishi mbali na hospitali ya
wilaya.
No comments:
Post a Comment