Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, wakisikiliza kwa makini maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao chao cha baraza la Madiwani kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imemrejesha kazini
Mhandisi wa idara ya maji wilayani humo Vivian Mndolwa huku akipewa adhabu ya kukatwa
na kupokea nusu ya sehemu ya mshahara wake katika kipindi cha mwaka mmoja.
Adhabu hiyo imetolewa juzi na baraza la Madiwani wa
halmashauri ya wilaya hiyo katika kikao chao kilichofanyika kwenye ukumbi wa
Umati mjini hapa ambapo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ambrose Nchimbi alisema
hayo mbele ya baraza hilo mara baada ya kuketi kikao cha kamati ya mamlaka ya nidhamu kwa
muda wa zaidi ya masaa matatu na kufikia muafaka wa kutoa adhabu hiyo.
Nchimbi alisema kuwa utekelezaji wa adhabu hiyo unaanza
mapema kuanzia sasa mwezi Agosti mwaka huu na kwamba inafuatia baada ya Mhandisi
huyo kupatikana na tuhuma ya kushindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa mradi wa
maji uliopo katika kitongoji cha Mnazi mmoja, kijiji cha Mkako kata ya Mkako
ambao unadaiwa kujengwa chini ya kiwango na kushindwa kuwafikishia maji
ipasavyo wananchi katika maeneo husika ndani ya kata hiyo.
Aidha Mndolwa hapo awali alisimamishwa kazi kufuatia agizo lililotolewa
Mei 8 mwaka huu na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad
Amour kwa kumtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kuunda kamati ambayo
ilifanya kazi ya kuchunguza tatizo hilo na baadaye hatua husika ziweze
kuchukuliwa dhidi ya wahusika waliohujumu mradi huo.
Pia mradi huo imeelezwa kuwa ulianza kujengwa Machi 28 mwaka
2014 kwa gharama ya shilingi milioni 718,896,533 chini ya ufadhili wa benki ya
dunia ambapo ilibidi ujenzi wake ukamilike katika kipindi cha mwaka mmoja tangu
uanze kujengwa, lakini hadi kufikia kipindi cha mwaka huu 2017 ujenzi huo bado
haujakamilika na fedha za mradi huo zimetumika katika kazi hiyo ya ujenzi.
Vilevile kampuni iliyohusika na kazi ya ujenzi huo imeelezwa
kuwa ni ya PATTY Interplan ya kutoka Jijini Dar es Salaam na kwamba tayari
halmashauri ya wilaya hiyo imevunja mkataba na mkandarasi huyo baada ya kuonekana
kumekuwa na ubabaishaji mkubwa juu ya ukamilishaji wa ujenzi wa mradi huo.
Mpaka sasa hatua ya ujenzi wa mradi huo yamejengwa matenki
mawili ya maji ikiwemo moja kubwa lenye ujazo wa lita 200,000 na lingine ndogo
lenye ujazo wa lita 75,000 ikiwemo ufukiaji chini wa mabomba ya Plastiki kutoka
kwenye chanzo kikuu cha kuleta maji katika matenki hayo.
Kadhalika vituo 36 vya kuchotea maji vimejengwa lakini
kutokana na ucheleweshaji wa ujenzi wa mradi huo na kuleta maji kwenye mabomba
hayo kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa kata ya Mkako wilayani Mbinga,
inadaiwa kuwa siku kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru alipowasili hapo
walipojaribu kuleta maji kwenye matenki hayo kwa ajili ya kupeleka kwenye vituo
hivyo vya kuchotea maji, mabomba hayo yalikuwa yamepasuka na kushindwa kupeleka
maji katika vituo hivyo jambo ambalo linadhihirisha wazi kuwa ujenzi wa mradi
huo ulikuwa ni wa chini ya kiwango.
Hivyo basi, Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga iliunda Kamati
maalumu ya watu saba ambayo ndiyo ilichunguza suala hilo ambayo ilitoka kwenye
vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya wilaya na wengine walikuwa ni wajumbe wa
ngazi ya halmashauri ya wilaya hiyo na kubaini kwamba ujenzi wake ulifanyika
chini ya kiwango.
No comments:
Post a Comment