Na Kassian Nyandindi,
Songea.
DOKTA Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
amepiga marufuku Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani humo, kubadilisha
matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi bila kuwa na kibali
maalum.
“Lazima tufuate kanuni na sheria zilizowekwa, huwezi
kubadilisha matumizi ya fedha kutoka sehemu fulani kwenda kwenye mradi fulani wa
maendeleo bila kibali maalum, cha msingi hapa ni lazima tufuate taratibu na
sheria zilizowekwa”, alisisitiza.
Alitoa onyo hilo juzi alipokuwa akifunga kikao cha
utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) mkoani humo kwa mwaka 2015/2016 kilichofanyika juzi kwenye
ukumbi wa Ikulu ndogo uliopo Songea mjini.
Dokta Mahenge alisema ni aibu na kosa kubwa kwa halmashauri
kuwa na hoja za muda mrefu za CAG ambazo hazijibiwi kwa wakati na kwamba
alisisitiza watendaji ndani ya halmashauri zao kuona umuhimu na kuipatia uzito
taarifa ya Mkaguzi huyo wa hesabu za serikali kwa kutekeleza maagizo yake kwa
wakati.
Vilevile alisema kuwa makundi ya vijana, walemavu, wanawake
na wazee yatengewe fedha kupitia vikundi vyao vya miradi ya maendeleo ambavyo
wamejiunga ili waweze kuondokana na umaskini.
Kadhalika alieleza pia Wakurugenzi hao wanapaswa kutenga maeneo
ya ujenzi wa viwanda katika halmashauri zao ambapo viongozi wote waliopo katika
eneo husika amewataka pia washirikiane katika utekelezaji wa jambo hilo ili
kuweza kuleta ufanisi mzuri.
No comments:
Post a Comment