Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga wakiwa katika kikao chao cha baraza la madiwani. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma limepitisha kwa pamoja na kukubaliana kwamba, ujenzi wa Ofisi za
makao makuu ya wilaya hiyo zitajengwa katika eneo maarufu linalofahamika kwa
jina la Ndengu lililopo katika kata Nyoni wilayani humo.
Maamuzi hayo yalifikiwa juzi katika kikao hicho
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa, baada ya uwepo wa mvutano
mkubwa uliodumu kwa masaa kadhaa kati ya Madiwani hao na Watendaji wa halmashauri
hiyo juu ya wapi Ofisi hizo zitajengwa.
Awali zilipopigwa kura kwa lengo la kukubaliana kwamba ujenzi
huo ukafanyike katika eneo la Kiamili lililopo katika kata ya Kigonsera,
Madiwani hao walikataa na kukubaliana kwamba zipigwe kura kwa mara ya pili kwa
kuchagua kati ya eneo la Maguu, Ndengu na Matiri.
Zilipopigwa kura kuchagua katika maeneo hayo ndipo waliweza
kuchagua eneo hilo la Ndengu ambalo lilishinda kwa kura 24, likifuatiwa na
Matiri kwa kura 9 na Maguu kwa kura 1 huku kura mbili zikiharibika kati ya wapiga
kura 36 waliokuwepo katika kikao hicho.
Matokeo hayo ya makubaliano wapi ukafanyike ujenzi wa Ofisi
hizo za makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga juu ya eneo hilo
lililoshinda kwa kura nyingi yalitangazwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
hiyo, Gombo Samandito mbele ya kikao cha baraza hilo mara baada ya uchaguzi huo
kufanyika.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kura za Ndengu ni 24 kwa hiyo napenda
kutangaza kwamba kwa mujibu wa kura hizi halali eneo la halmashauri kuu ya
wilaya yetu litakuwa ni Ndengu”, alisema Samandito.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Ambrose
Nchimbi aliongeza kuwa yeye anaamini kwamba miundombinu ya majengo ya
halmashauri hiyo itakapojengwa hapo itakaa vizuri na kwamba watakachokifanya ni
kuongea na Wizara husika ili iweze kutangaza eneo hilo kwamba sasa linafaa kwa kujengwa
makao makuu ya wilaya hiyo.
“Kura ambazo Ndengu tumezitoa ninahakika kabisa sasa ugomvi
umekwisha tubaki Madiwani kuwa wamoja juu ya kukamilisha zoezi hili la ujenzi
wa miundombinu hii ya halmashauri yetu”, alisisitiza Nchimbi.
Pamoja na mambo mengine, kwa ujumla halmashauri hiyo imefikia
hatua ya kuhama katika Ofisi zake za awali zilizopo mjini hapa na kwenda
kujenga miundombinu mingine mipya ya wilaya hiyo, baada ya kugawika na kuizaa
halmashauri nyingine ya mji wa Mbinga ambayo ndiyo inapaswa kutumia majengo
hayo yaliyopo sasa mjini hapa.
No comments:
Post a Comment