Wataalamu wa Manispaa ya Songea wakikagua moja kati ya barabara ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Benki ya dunia. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MANISPAA ya Songea mkoani Ruvuma inatarajia kutumia zaidi ya
shilingi bilioni 14.320 katika ujenzi wa barabara zake za mji huo kwa kiwango
cha lami zenye urefu wa kilometa 8.6.
Afisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa fedha
za mradi huo zimetolewa na Benki ya dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo
serikali za mitaa (ULGSP) kwa lengo la kuendeleza miundombinu ya halmashauri za
Miji na Manispaa 18 zilizopo Tanzania bara ikiwemo Manispaa hiyo ya Songea.
Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi mwaka 2015 alieleza kuwa ulitarajiwa
kukamilika Juni 30 mwaka huu ambapo awali fedha iliyopokelewa na Manispaa hiyo
ilikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni saba ambayo imeanza kutekeleza mradi huo
ambapo hadi sasa mkandarasi husika amekwisha lipwa kwanza shilingi bilioni nne.
Alifafanua kuwa barabara za Manispaa ya Songea ambazo zipo
kwenye mradi huo ni kuanzia maeneo ya mtaa wa FFU hadi Matogoro yenye urefu wa
kilometa 3.2, barabara ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5
na barabara ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.
Midelo aliongeza kuwa nyingine ni ya kutoka mtaa wa Mitumbani
hadi Yapenda yenye urefu wa kilometa moja, barabara ya Polisi hadi Stendi ya
Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.
Hata hivyo muda wa kumaliza kazi kwa Mkandarasi ulikuwa ni tangu
mwezi Juni 30 mwaka huu ambapo kufuatia hali hiyo tayari Mkandarasi huyo ameingizwa
kwenye tozo (Liquidated Damage) na kwamba iwapo atashindwa kumaliza kazi kwa
siku 100 hatua za kisheria za kuvunja mkataba wake zitafanyika.
No comments:
Post a Comment