Tuesday, August 1, 2017

WANAFUNZI MASUMUNI HALMASHAURI MJI WA MBINGA WALALAMIKIA MAJENGO WANAYOSOMEA KUTOFANYIWA UKARABATI MIAKA MINGI

Hili ni moja kati ya jengo la shule ya msingi Masumuni ambalo hivi sasa limefungwa watoto wasiendelee kulitumia wakati wa vipindi vya masomo wanapokuwa darasani kutokana na jengo hilo kuwa katika hali mbaya. 
Majengo hayo ya madarasa kwa ndani yanavyoonesha kuwa ni chakavu na yamejenga nyufa kubwa ambazo zinahatarisha usalama wa wanafunzi na walimu wanapokuwa kwenye vipindi vya masomo. 
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

WANAFUNZI wanaosoma katika shule ya msingi Masumuni Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma wamelalamikia kitendo cha halmashauri hiyo kwa kutochukua hatua za haraka kuyafanyia ukarabati majengo ya vyumba vitano vya madarasa wanayosomea, ambayo yamejenga nyufa kubwa na kuanza kubomoka hali ambayo inawafanya kuwa katika mazingira magumu ya kusomea wakati wanapokuwa kwenye vipindi vya masomo darasani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi walidai kuwa tokea mwaka 2011 vyumba hivyo vya madarasa vimebomoka hakuna hatua zilizochukuliwa, jambo ambalo linahatarisha hali ya usalama wao hivyo wanaiomba serikali kulipatia kipaumbele suala hilo kwa kuyafanyia ukarabati mapema ili waweze kuondokana na adha hiyo wanayoipata sasa.

Shule hiyo ambayo pia inajumla ya vyumba tisa vya madarasa na wanafunzi 800 wakiwemo wanaume 392 na wanawake 408 wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao walieleza kuwa uongozi wa halmashauri ya mji huo kupitia idara yake ya elimu msingi, ilikwisha toa ushauri kwamba majengo hayo sio rafiki kwa matumizi ya binadamu ambapo kufuatia hali hiyo siku kadhaa zilizopita wamechukua hatua ya kuyafungia madarasa hayo ili wanafunzi wasiweze kuyatumia hadi hapo yatakapofanyiwa ukarabati.


“Madarasa ambayo ni mabovu katika vyumba hivi vitano yalikuwa yakitumika kusomea wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza, la pili na la nne majengo haya tumepigwa marufuku kuyatumia alifika hapa shuleni mtaalamu wa majengo na kuyaangalia jinsi yalivyo hivyo akapiga marufuku tusiyatumie na sasa tunalazimika kuingia kwa zamu kwa kutumia majengo mengine yaliyopo hapa shuleni hali ambayo inatufanya tushindwe kuhudhuria vipindi vya masomo darasani ipasavyo”, walisema.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Masumuni, Yordan Ndunguru alipozungumza na mwandishi wa habari hizi shuleni hapo alithibitisha kuwepo kwa hali hiyo na kueleza kuwa mazingira ya kusomea watoto hao sio rafiki yanawafanya hata wafikie hatua ya kuhama kwenda shule nyingine zilizokuwa nje ya maeneo yao wanayoishi kutokana na shule hiyo kuwa katika hali mbaya.

“Changamoto kubwa inayopatikana hapa, watoto hawa wanakosa haki yao ya msingi ya kupata taaluma na vipindi vya masomo havifundishwi ipasavyo kutokana na kusoma kwa zamu kwa kutumia madarasa mengine”, alisema Ndunguru.

Pia aliongeza kuwa hali hiyo inawafanya hata wanafunzi wake wawe wazururaji na maadili yao kuharibika kutokana na wakati mwingine muda mwingi hukaa majumbani kutokana na kukosa sehemu ya kusomea.

Naye diwani wa kata ya Masumuni Raphael Kambanga alipohojiwa na mwandishi wetu alisema kuwa tatizo hilo amelipigia kelele kwa muda mrefu katika vikao husika, lakini serikali kupitia Mkurugenzi wake wa halmashauri ya mji wa Mbinga Robert Mageni hakuna hatua zozote zilizochukuliwa juu ya ukarabati wa majengo hayo.

Kambanga alibainisha kuwa uongozi wa mji na jamii kwa ujumla inapaswa kuliona tatizo hilo na kulipatia kipaumbele ukizingatia kwamba shule hiyo ipo katikati ya mji wa Mbinga, hivyo wanapaswa kushirikiana pamoja katika kuimarisha miundombinu yake ili kuweza kuondoa hata matatizo ya utoro kwa watoto wanaosoma shuleni hapo.

Pamoja na mambo mengine, juzi katika kikao cha baraza la Madiwani Mkurugenzi huyo mtendaji wa halmashauri ya mji huo alilieleza baraza hilo kuwa wameshindwa kuyakarabati majengo hayo kutokana na kukosa fedha hivyo katika bajeti ya maendeleo mwaka huu wa 2017/2018 wametenga fedha ili kuweza kuyafanyia ukarabati na watoto hao waweze kusoma wakiwa katika mazingira mazuri.

 


No comments: