Wananchi wakiwa katika eneo la tukio wakati miili ya wanafunzi wa shule ya msingi Chikomo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ikitafutwa baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo wakati wakichimba mchanga. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANAFUNZI wawili wanaosoma katika shule ya msingi Chikomo iliyopo
katika kata ya Mbesa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamefariki dunia baada ya
kuangukiwa na kifusi cha udongo wakati wakichimba mchanga.
Tukio hilo lilitokea Agosti 15 mwaka huu na kwamba katika
tukio hilo wanafunzi hao walikuwa wakichimba mchanga kwa ajili ya matumizi ya
ujenzi wa darasa katika shule yao.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Kamishina Mwandamizi wa
Polisi, Gemini Mushi aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Sophia Ngongi na Semen
Selemani wote wanaosoma darasa la tatu katika shule hiyo.
Akizungumzia tukio hilo Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Omary Melle
alisema kuwa tukio ajali hilo lilitokea majira ya saa 9:20 baada ya wanafunzi
hao wakiwa wametoka darasani muda wa masomo kwisha.
Melle alisema shule yake imekuwa ikiwatumia wanafunzi wa
shule ya msingi Chikomo kusomba mchanga kutokana na wazazi na walezi wa watoto wanaosoma
katika shule hiyo kugoma kufanya kazi za kujitolea ili kufanikisha ujenzi wa
darasa linalojengwa shuleni hapo.
Wakisimulia mkasa huo Afisa mtendaji wa kata ya Mbesa, Raso
Kundete na diwani wa kata hiyo, Abdul Mfaume walisema kuwa wanafunzi hao
walipiga kelele kwa ajili ya kuomba msaada wakati tukio hilo linatokea na
baadaye watu walienda katika eneo la tukio kwa ajili ya kuwaokoa lakini
ilishindikana kuokoa uhai wao.
Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi wa shule hiyo, Hassan Nasoro
alithibitisha kutolewa mamlaka kwa walimu hao kuwatumia wanafunzi wa shule hiyo
kubeba mchanga ili kuharakisha ujenzi wa darasa hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa kijiji
hicho waliwatuhumu walimu hao kuwa wamekuwa na tabia ya kuwatumikisha watoto
wao bila kufuata taratibu husika.
Akifafanua taarifa hiyo Mwenyekiti wa kijiji cha Chikomo,
Mitawa Adam alisema kuwa wanafunzi hao walianza kubebeshwa mchanga huo bila
kutoa taarifa yoyote kwa viongozi wao wa vijiji.
Alisema kuwa wananchi wa kijiji chake ni wasikivu na ndiyo
maana walikubali kujitolea kufyatua tofari 135, 000 ambayo hivi sasa yanatumiwa
kwa ajili ya ujenzi wa darasa hilo.
Mganga aliyeifanyia uchunguzi miili ya wanafunzi waliopoteza
maisha katika tukio hilo, Dokta Andreas Ndunguru alisema kuwa chanzo cha kifo
hicho kilitokana na wanafunzi hao kukosa hewa baada ya kufunikwa na kifusi cha
udongo huo.
No comments:
Post a Comment