Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge akitoa maagizo juu ya kusitisha huduma ya maji kwa idara na taasisi zote za umma zilizopo katika Manispaa ya Songea. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge ameiagiza
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Songea (SOUWASA) kusitisha mara
moja huduma ya maji kwa idara na taasisi zote za umma zilizopo chini ya Manispaa ya
Songea kutokana na deni kubwa la huduma ya maji, lililofikia zaidi ya shilingi
milioni 6,574,686.79 ambazo Manispaa hiyo haijaonesha dalili za kulipa deni
hilo.
Akizungumza juzi katika kikao maalumu kati ya
viongozi wa SOUWASA na uongozi wa Manispaa hiyo uliowakilishwa na Mhandisi wa
maji, Samwel Sanya Dokta Mahenge alisema kuwa amelazimika kutoa agizo
hilo baada ya kuchoshwa na tabia ya viongozi wake kutoonesha
ushirikiano licha ya kupewa taarifa ya kuwataka kulipa fedha kwa mamlaka hiyo.
Dokta Mahenge alisema kuwa amechoshwa na tabia ya uongozi wa
Manispaa ya Songea chini ya Mkurugenzi wake Tina Sekambo, ambaye mara kwa mara
ameonekana kukaidi na kudharau hata maagizo ya viongozi wake wa juu ikiwemo juu
ya kulipa madeni ya Wenyeviti wa mitaa ambao wamekuwa msaada mkubwa katika shughuli
za kukusanya mapato na ulinzi katika mitaa yao.
“Ninyi Manispaa ya Songea mnatia aibu sana, naagiza kuanzia
leo natoa siku saba kwa Mamlaka hii ya maji kuwakatia huduma ya maji katika
taasisi zenu zote kama hamtalipa deni mnalodaiwa, mbona umeme mnalipa na
hamtaki kulipia huduma ya maji ambayo kwenu ni muhimu”, alihoji Dokta Mahenge.
Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Mahenge alikwenda mbali
zaidi na kusisitiza kuwa licha ya Manispaa hiyo kuwa na vyanzo vingi vinavyoiingizia mapato,
lakini ndiyo inayoongoza kwa madeni na kuwaagiza kulipa madeni yote
wanayodaiwa na watu mbalimbali.
Alisema kuwa inasikitisha kuona kila kukicha Manispaa imekuwa
ikilalamikiwa na watoa huduma, hata hivyo Mkurugenzi wake amekuwa akionyesha
dharau ya maagizo kutoka kwa viongozi na manispaa imeonekana imezoea kudaiwa
madeni na watu pamoja na taasisi nyingine za serikali zinazotoa huduma.
Vilevile ameitaka Mamlaka hiyo ya maji safi na usafi wa
mazingira mjini Songea kuchukua hatua kwa wadaiwa wote sugu na kutowaonea
huruma kwani endapo wakiendekeza huruma hawataweza kupata fedha wanazodai jambo
ambalo litarudisha nyuma juhudi na mikakati yao ya kuongeza mapato na kuboresha
huduma zake kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment