Na Mwandishi wetu,
Songea.
MKOA wa Ruvuma umetajwa kuwa ni miongoni mwa mikoa michache
hapa nchini ambayo inazalisha zao la Soya kwa wingi, huku changamoto kubwa
ikiwa ni ukosefu wa soko la uhakika licha ya uzalishaji wake kuongezeka mwaka
hadi mwaka.
Dokta Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma
alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akifungua kikao cha Wadau wa zao hilo
ambacho kilijumuisha mikoa mitatu ya Ruvuma, Iringa na Njombe
kilichofanyika katika Manispaa ya Songea mkoani hapa.
Alisema uzalishaji wa Soya umekuwa ukiongezeka toka msimu wa
2014/2015 na msimu wa mwaka 2016/2017 ambapo ulizalisha hekta
33,267 zilizoweza kutoa tani 32,331 ukilinganisha na msimu wa mwaka 2015/2016
ambao kulikuwa na hekta 19,026 zilizotoa tani 16,754.
Hilo ni ongezeko la ukubwa wa hekta 14,241 na uzalishaji wa
tani 15,577 sawa na ongezeko la asilimia 48 ya uzalishaji kwa msimu wa
2015/2016 ambalo linaonesha jinsi gani wakulima wa mkoa huo walivyohamasika
kulima zao hilo.
Dokta Mahenge alifafanua kuwa changamoto kubwa inayowakabili
wakulima hao ni soko la kuuzia zao hilo ambapo hivi sasa kuna kampuni moja ya
Silverlands ambayo hupita kununua kupitia wakulima waliopo kwenye vikundi huku
mkulima mmoja mmoja akiuza kwa kampuni binafsi ya Export Trade Company
Limited.
Aliongeza kuwa tatizo kubwa lingine wanalokabiliana nalo
wakulima hao mazao yao kutonunuliwa kwa wakati baada ya kuyakusanya kwenye
maghala ambako wanayahifadhi.
Kwa upande wake mwakilishi wa mpango wa kuendeleza kilimo cha
mazao mbalimbali katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (Sagcot) Maria Jumba
alisema kuwa kuna maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya kuendeleza shughuli
za kilimo katika ukanda wa mikoa ya nyanda za juu kusini ikiwemo Ruvuma.
Hivyo basi alisema kuwa kazi kubwa ya Sagcot ni kuratibu
malengo mahususi ili kuweza kuleta tija kupitia shughuli za kilimo katika
ukanda fulani na kutoa kushauri kwa wakulima ili kuongezeka uzalishaji hasa
baada ya soko la Tanzania kufunguka na kuwepo kwa makubaliano ya kibiashara na
nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Maria aliwaasa Watanzania kutoogopa ushindani wa kibiashara
badala yake kutumia fursa iliyopo kujikita zaidi kwa kuzalisha bidhaa bora
zitakazoweza kuingia katika soko la ushindani.
No comments:
Post a Comment