Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
CHAMA cha ushirika Mbinga Walimu SACCOS kilichopo wilayani Mbinga
mkoa wa Ruvuma kimepata hasara ya shilingi bilioni 1,033,002,579 ambazo
zilitokana na akiba, hisa na amana za wanachama jambo ambalo hivi sasa limesababisha chama hicho
kushindwa kujiendesha kwa manufaa ya wanachama wake.
Aidha kufuatia hali hiyo wanachama hao wamekubaliana kwamba viongozi
wa bodi na watendaji wake walioshiriki kukihujumu na kusababisha hasara hiyo wachukuliwe
hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani ili waweze kulipa fedha hizo.
Makubaliano hayo ya wanachama hao yalifikiwa katika mkutano
wao maalumu ulioketi jana kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa
mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye.
Akisoma taarifa ya ukaguzi ya SACCOS hiyo mbele ya Mkuu huyo
wa wilaya mmoja kati ya wajumbe wa bodi ya mpito ambayo iliteuliwa kwa muda kusimamia
na kuongoza chama hicho, Judith Komba alisema kuwa mpaka kufikia Septemba 26
mwaka jana chama ilibidi kiwepo na fedha hizo lakini hakina fedha kutokana na
matumizi mabaya yaliyokuwa yakifanyika na viongozi wa bodi na watendaji wake waliokuwepo
hapo awali.
Alifafanua kuwa fedha hizo ambazo wanadaiwa kujinufaisha kwa
matakwa yao binafsi zimetokana na akiba za wanachama ambazo zilitakiwa kuwepo shilingi
milioni 929,091,579, hisa shilingi milioni 90,760,000 na amana shilingi milioni
13,151,000 lakini kumekuwa na mbinu chafu ambazo zilikuwa zikitumika kutengeneza
mikopo hewa isiyofuata taratibu ndiyo maana hasara hiyo imejitokeza ndani ya
chama.
Komba alieleza kuwa bodi hiyo na watendaji hao wamesababisha pia
mikopo hiyo kutolewa bila kujali hisa na akiba alizonazo mwanachama hivyo
kusababisha hata mkopo husika kushindwa kurejeshwa kupitia makato yanayokatwa
katika mfumo unaozingatia theluthi tatu ya mshahara wa mkopaji.
Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo ya mpito Mbinga Walimu SACCOS,
Vitalis Mapunda aliwataja wanaonyoshewa kidole wakidaiwa kuhusika juu ya upotevu
wa fedha hizo za wanachama kuwa ni Sostenes Ndunguru ambaye alikuwa Meneja, Stephen
Komba mjumbe kamati ya usimamizi na Edmund Hyera ambaye alikuwa ni mjumbe wa
bodi.
Vilevile wengine ni Emmanuel Kapinga aliyekuwa Mwenyekiti,
Kenneth Ndunguru, John Komba, Peter Challe, Batson Mpogolo, Osmund Komba, Wille
Mkwene, Marion Nchillas, Materinus Ndunguru na Tabu Mshani, Menas Matembo,
Gervas Kapinga, Osmund Kihwili, Salvanus Hyera, Samwel Maridadi, Mary Nchimbi
na Sadick Mango ambao wote nao walikuwa ni wajumbe wa bodi katika SACCOS hiyo.
Awali kwa upande wake akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa
wilaya ya Mbinga, Nshenye alisema kuwa yeye ofisi yake haitaweza kuvumilia
vitendo hivyo vya wizi wa fedha za wananchama hao na kwamba amewataka wale wote
waliohusika kuchukua fedha hizo bila kufuata taratibu wazirejeshe mapema iwezekanavyo
kabla hawajachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Mimi sina hiyo huruma kwa sababu kama umevunja sheria
haijalishi wewe ni mtumishi au sio mtumishi, kwangu hawa wahalifu siwahitaji
mimi natoa agizo watafutwe popote walipo waitwe walipe fedha hizi kabla hatua
nyingine hazijachukuliwa”, alisisitiza Nshenye.
Kadhalika kufuatia kuwepo kwa hali hiyo pia Nshenye alitoa onyo
kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika wilayani humo kuacha mara moja vitendo
vya wizi wa fedha na mali za ushirika.
Nao wakichangia hoja kwa nyakati tofauti katika mkutano huo
wanachama wa SACCOS hiyo waliunga mkono jitihada hizo wakisema kuwa wale wote
ambao wanadaiwa na chama hicho wakamatwe na endapo kama wanakaidi kurejesha fedha
hizo wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Walisema wamesikitishwa na taarifa hizo ambazo zinaonesha
kuwa ni utovu mkubwa wa nidhamu uliofanyika ndani ya chama chao juu ya matumizi
mabaya ya fedha za wanachama.
Inosensia Nombo ambaye ni mmoja kati ya wanachama wa ushirika
huo aliongeza kuwa taarifa hiyo ya ukaguzi ambayo ilisomwa mbele yao inaonesha
kuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha na dosari nyingi za kiutendaji, hivyo kuna
kila sababu kwa viongozi waliohusika kuchukuliwa hatua ili iweze kuwa mfano na
fundisho kwa wengine.
Pia Gerald Ndunguru naye alisema; “wakati najiwekea akiba
mpaka nafikia hatua ya kustaafu haki zangu sijazipata kwa kilio hiki
kilichotupata, hawa watuhumiwa wanastahili kabisa kukamatwa na kutiwa pingu
mikononi ili wafikishwe mahakamani kwani inasikitisha na kutuongezea uchungu
mkubwa katika maisha yetu”.
Hata hivyo pamoja na mambo mengine, chama cha ushirika Mbinga
Walimu SACCOS kinaundwa na wanachama ambao ni watumishi wa serikali wanaotoka katika
halmashauri ya mji wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa ambapo makao makuu ya ofisi
zake yapo Mbinga mjini.
No comments:
Post a Comment