Na Mwandishi wetu,
MKEMIA kutoka
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali, Elias Mulima ameiambia Mahakama ya Hakimu mkazi
Kisutu kuwa sampuli ya mkojo wa msanii Agnes Gerald maarufu kama Deal ama
Masogange (28) umebainika kuwa na dawa ya kulevya aina ya Heroin.
Akitoa ushahidi
huo leo Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, shahidi huyo wa
kwanza wa upande wa mashtaka akiongozwa na Wakili wa serikali, Constantine
Kakula alisema kuwa February 15 mwaka huu askari wawili kutoka Jeshi la Polisi
hapa nchini Koplo Sospeter na WP Judith, walimfikisha Masogange ofisini kwake
kwa lengo la kumfanyia vipimo vya mkojo wake.
Agness Masogange. |
Baada ya
kuwapokea, alimsajili Masogange na kumpa namba ya maabara 446/2017 na kisha
kuwakabidhi kifaa maalum kwa ajili ya kuweka sampuli hizo za mkojo.
Alidai baada ya
kupokea sampuli hizo, Masogange alifanyiwa uchunguzi kwa kutumia kemikali na
kubaini kuwa mkojo wake una chembechembe za dawa za kulevya aina ya Heroin
ambazo kwa kitaalamu zinajulikana kama Diacety Imophine.
Kadhalika uchunguzi
zaidi unaeleza na kufafanua kuwa chembechembe hizo za dawa nyingine ya kulevya ni
aina ya Oxazepam.
Shahidi huyo
alidai kuwa baada ya kufanya uchunguzi huo aliandaa taarifa ya uchunguzi
kuhusiana na sampuli hiyo ya mkojo ambapo aliisaini yeye mwenyewe na kuthibitishwa
juu ya madawa hayo ya kulevya na kwamba shahidi huyo alimtambua Masogange kuwa
ndiye aliyepelekwa kuchukuliwa sampuli hiyo ya mkojo ofisini kwake.
Vilevile alidai
kuwa anaweza kuitambua taarifa hiyo ya uchunguzi kutokana na kuwepo kwa saini
yake, muhuri wa moto wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali ambapo ameomba Mahakama
kupokea vitu hivyo kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.
Mawakili
Nehemiah Nkoko na Reuben Simwanza ambao wanamtetea Masogange wamepinga taarifa
hiyo ya uchunguzi wakitaka isipokelewe na Mahakama hiyo kwa madai kwamba haijakidhi
vigezo vya kisheria.
Nkoko alidai kuwa
utaratibu wa kisheria haukufuatwa kabla ya mtuhumiwa alipokuwa chini ya Polisi
kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, kwa kuwa ofisa wa Polisi alitakiwa kuwasilisha
maombi Mahakamani ndipo amri ya kupimwa itolewe.
“Ripoti ipo
kinyume na sheria Mahakama ina njia moja tu nayo ni kuikataa na sio kuikubali,
sheria ipo wazi tunaomba Mahakama ikubali pingamizi letu na kukataa kupokea
taarifa hiyo”, alisisitiza.
Naye Wakili
Simwanza alidai ripoti hiyo ikitazamwa inataja fomu nyingine ya ombi la Jeshi
la Polisi kwenda kwa Mkemia mkuu kwa ajili ya kufanya vipimo huku akidai kuwa ripoti
hiyo ipo yenyewe bila ya kuambatanishwa na fomu maalum inayotumiwa na Polisi
kupeleka sampuli hivyo haiwezi kupokelewa na kutumika kama kielelezo.
Akijibu hoja
hizo, Wakili Kakula alidai pingamizi hilo halina mashiko wala miguu ya
kusimamia kwani fomu ambayo haijaambatanishwa na ile ya mkemia mkuu ni vitu
viwili tofauti na hata uwasilishwaji wake unafanywa na watu wawili tofauti.
Kaukala
alifafanua kuwa taarifa ya mkemia inawasilishwa na mkemia na ile ya Polisi
inawasilishwa na Polisi ambapo kuhusu hoja ya sampuli ya mkojo, Wakili huyo alidai
kuwa kifungu cha 63 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA), kimeweka
mazingira ambayo ofisa wa Polisi atawasilisha maombi Mahakamani kuweza kuchukua
sampuli.
Pamoja na mambo mengine endapo mtuhumiwa anakataa kuchukuliwa sampuli ya
mkojo, hivyo atawasilisha ombi Mahakamani ili iweze kutolewa amri, hivyo Kakula
alisema katika pingamizi lao upande wa utetezi haujaeleza kwamba mshitakiwa
alikataa kupima au alilazimishwa na kwamba aliomba pingamizi hizo zitupiliwe
mbali.
Hakimu Mashauri
aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 28 mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa kupokelewa
kwa taarifa hiyo au la, Masogange amefikishwa Mahakamani hapo akidaiwa kutumia
dawa za kulevya aina ya Heroin kati ya Februari 7 na 14 mwaka huu katika maeneo
yasiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam
hata hivyo yupo nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment