Na Steven Augustino,
Tunduru.
WATEJA 456 waliopo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameweza
kupatiwa msaada wa kisheria katika nyanja ya usuluhishi wa migogoro mbalimbali
na kuwezeshwa kupata haki zao za msingi baada ya kuhitilafiana kwa muda mrefu.
Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la serikali wilayani humo,
Tunduru Paralegar Center (TUPACE) John Nginga alisema hayo alipokuwa akitoa
taarifa yake ya utekelezaji kwa Mkuu wa wilaya hiyo, Juma Homera.
Taarifa hiyo ilikuwa ikitolewa juzi wakati wa uzinduzi wa
mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma na uwajibikaji wa
viongozi wa serikali kwa wananchi uliofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya
wilaya hiyo uliopo mjini hapa.
Nginga alifafanua kuwa kati ya wahanga hao idadi ya wanawake
waliopatiwa msaada huo walikuwa 263 na wanaume ni 193.
Alisema kuwa miongoni mwa migogoro iliyopatiwa ufumbuzi na
shirika hilo sehemu kubwa ilikuwa ikihusisha ardhi za mashamba na maeneo ya
ujenzi wa nyumba na kwamba wanaendelea kufanya utafiti zaidi, ili kuweza
kubaini ni kwa kiasi gani kuna matukio ya migogoro ya ndoa na ukatili wa
kijinsia ingawa zipo taarifa kuna matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia.
Awali akisoma taarifa ya uzinduzi wa mafunzo ambayo
yaliwashirikisha viongozi wa kutoka katika kata ya Ligomba, Mlingoti mashariki,
Nakapanya na Majengo wilayani humo Furkon Makota alisema yameweza kuwajengea
uwezo wa kuibua changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi.
Makota alisema kuwa hali hiyo imeweza kubaini pia kuwepo kwa
ombwe kubwa kwa wananchi kutofahamu haki zao za msingi.
Akizungumzia hilo kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma Juma Homera pamoja na mambo mengine aliwataka washiriki wa mafunzo hayo
kutumia vyema elimu waliyoipata ili waweze kuisaidia wilaya hiyo katika kupiga
hatua mbalimbali za maendeleo.
Homera alieleza kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni pamoja na
kufanya utafiti na kutatua kero zote wanazokabiliana nazo wananchi hususani
zilizopo katika sekta ya kilimo katika miradi ya usambazaji wa pembejeo katika
kilimo cha zao la korosho.
Naye Afisa kilimo wa wilaya hiyo Yona Mwakatuma aliongeza
kuwa mbali na serikali kutoa pembejeo hizo ikiwemo madawa ya kupulizia
mikorosho kwa wakulima wilayani hapa kumekuwa pia na changamoto nyingi ikiwemo
ukosefu wa soko la uhakika la kuuzia zao hilo.
No comments:
Post a Comment