Baadhi ya washiriki wakiwa katika kikao cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoani Ruvuma. |
Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
IMEELEZWA kuwa Halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani
Ruvuma zisipoweka udhibiti wa kutosha katika eneo la manunuzi zitaendelea
kuisababishia hasara serikali, hivyo zimetakiwa kuboresha udhibiti huo hasa
kwenye kipengele cha manunuzi ya umma na kuweza kuimarisha ipasavyo miradi ya
maendeleo ya wananchi.
Aidha kila Mkurugenzi katika halmashauri hizo ameagizwa
kuwawezesha na kuwatumia wakaguzi wa ndani kikamilifu katika kutathimini
ufanisi wa mifumo ya udhibiti wa ndani na kuchukua hatua stahiki, sambamba na
kuziwezesha kamati za ukaguzi katika kutekeleza majukumu yao.
Mkuu wa mkoa huo, Dokta Binilith Mahenge alisema hayo wakati
alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2015/2016
kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Ikulu ndogo mjini hapa.
“Katika eneo hili nataka kila halmashauri iendelee kuchukua
hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi watakaobainika kuhusika na vitendo vya
ubadhirifu au kutowajibika ipasavyo na kuisababishia hasara serikali”, alisema
Dokta Mahenge.
Dokta Mahenge aliongeza kuwa kufanyika kwa kikao hicho ni
muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambayo
yanawataka Wakurugenzi wote katika halmashauri kuhakikisha kwamba hoja na
mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinajadiliwa na
hatua za kisheria na nidhamu zinachukuliwa kwa wakati dhidi ya wale wote ambao
kwa namna moja au nyingine wameshiriki kuwepo kwa hujuma mbalimbali.
Pia alisisitiza kuwa ni wajibu kwa kila Mkurugenzi kwa
kushirikiana na Madiwani wahakikishe mifumo ya hoja za miaka ya nyuma kwa kila
mwaka wa fedha zinajibiwa ipasavyo na kufungwa kwa wakati.
Naye Mwakilishi wa CAG mkoani Ruvuma, Suleiman Mwaliwale
akizungumza katika kikao hicho alieleza kuwa wameweza kubaini mapungufu
mbalimbali ndani ya halmashauri ikiwemo kutokuwa na mifumo mizuri ya ndani ya
udhibiti na ukusanyaji wa mapato, michakato ya uteuzi wa wakandarasi kutofuata
taratibu husika na kusababisha miradi ya maendeleleo ya wananchi kutekelezwa
chini ya kiwango.
Alisema kumekuwa pia na udhaifu wa ukaguzi wa vitengo vya
ndani ambapo hali hiyo inasababishwa na uhaba wa rasilimali watu na kutengewa
fedha bajeti ndogo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Pamoja na mambo mengine, wakichangia hoja kwa nyakati tofauti
wajumbe waliohudhuria kikao hicho walimweleza Mkuu wa mkoa huo Dokta Mahenge
kwamba watatekeleza maagizo ya serikali ipasavyo na kurekebisha kasoro zilizopo
ili zisiweze kujirudia tena katika mwaka wa fedha ujao.
Hata hivyo kikao hicho cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali hapa mkoani Ruvuma kilihusisha viongozi wake wa kutoka ndani ya halmashauri
za mkoa huo ambazo ni wilaya ya Songea, Mbinga, Namtumbo, Tunduru na Manispaa
ya Songea.
No comments:
Post a Comment