Monday, August 21, 2017

MBIO ZA MARATHON SELOU NAMTUMBO KUFANYIKA SEPTEMBA MWAKA HUU

Na Mwandishi wetu,    
Namtumbo.

KAMPUNI tanzu ya Mantra inayochimba madini ya Uranium One na ROSATOM wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, imedhamini mbio za Marathon Selou Namtumbo ambazo zinatarajiwa kuanza kufanyika mapema mwezi Septemba mwaka huu.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Mkuu wa wilaya ya hiyo, Luckness Amlima alisema kuwa mbio hizo zitakuwa za urefu wa kilometa 2.5 kwa wanawake, kilometa tano kwa wanawake na wanaume na kilometa 21 kwa wanawake na wanaume ambapo zina lenga kuhamasisha michezo na kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanawake na jengo la upasuaji wilayani hapa.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa lengo ni kukusanya shilingi bilioni 7 ambazo kama zitapatikana zitaweza pia kutosheleza kujenga hospitali ya wilaya ya Namtumbo.


Vilevile katika mashindano hayo wanategemea kukusanya fedha za awali shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kuanzia ujenzi wa wodi ya akina mama wajawazito na chumba cha upasuaji.

Alisema kuwa tayari washiriki wa kutoka ndani na nje ya nchi kama vile Urusi, Afrika Kusini na Kazastan wameonesha nia ya kushiriki mbio hizo ambapo gharama ya kushiriki kwa mtu mmoja ni shilingi 5,000 kwa kilometa 2.5 na kwa wale watakaokimbia kilometa 5 na 21 watatakiwa kulipa shilingi 10,000 ambapo washiriki wa kutoka nje ya nchi watalipiwa na makampuni yao.

Mbali na kukusanya fedha hizo kwa ajili ya kuchangia huduma za afya pia mkakati mwingine ni kuitangaza mbunga maarufu ya Selou, ambayo inapatikana katika wilaya hiyo ya Namtumbo na kwamba washiriki wengine katika mbio hizo watakuwa Wenyeviti wa halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma, Wakurugenzi watendaji, Wakuu wa wilaya ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge.


Kwa upande wake Meneja mahusiano na mawasiliano wa Mantra, Khadija Palangyo alisema kuwa mbio hizo zitaanzia katika jengo linalotumika kama hospitali ya wilaya ya Namtumbo na wakimbiaji wa mbio hizo watapewa zawadi za aina mbalimbali.

No comments: