Tuesday, August 29, 2017

RUVUMA KUONGEZA IDADI YA VITUO UPIMAJI SARATANI SHINGO YA KIZAZI

Na Mwandishi wetu,   
Songea.

ONGEZEKO la magonjwa yasiyoambukizwa katika mkoa wa Ruvuma imeelezwa kuwa yanasababishwa kwa kiasi kikubwa na mfumo wa maisha wanayoishi wananchi wa mkoa huo pamoja na ongezeko la watu wenye umri mkubwa katika jamii.

Aidha kutoshiriki mazoezi ya kimwili, ulaji wa mbogamboga, matunda na utumiaji wa pombe kupita kiasi nao umekuwa ukichangia wananchi kupata magonjwa hayo.

Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dokta Gozibert Mutangabarwa alisema hayo juzi alipokuwa akitoa taarifa juu ya hali ya tatizo la maradhi ya Saratani ya mlango wa kizazi na matiti,


Kifua kikuu, shinikizo la damu na sukari wakati wa mpango zoezi la ushauri na upimaji wa magonjwa hayo ulioratibiwa na Chama Cha Madaktari Wanawake (MEWATA) hapa nchini ambao unafanyika kwenye viwanja vya Majimaji mjini Songea.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo mkoa wa Ruvuma ambao hivi sasa una vituo 10 vinavyotoa huduma ya upimaji Saratani ya shingo ya kizazi pia wanalenga kuongeza idadi ya vituo kutoka asilimia nne hadi kufikia 60 ifikapo mwaka 2020.

Magonjwa mengine kama vile kifua kikuu na ukoma alieleza kuwa yamekuwa yakiongoza watu wengi kupoteza maisha hivyo serikali ya mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto kupitia mpango wa taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma wamekuwa wakifanya jitihada ya kupunguza magonjwa hayo licha ya kuwepo kwa changamoto kubwa ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Dokta Gozibert aliongeza kuwa katika kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo matibabu ya wagonjwa hao kwa asilimia 93 kwa halmashauri zote zilizopo ndani ya mkoa huo.

No comments: