Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifanya mazungumzo ya kikazi na Makamu wa Rais wa Cuba, Gladys Bejarano katika mji wa Havana nchini Cuba jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) |
Na Mwandishi wetu,
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo
na Makamu wa Rais wa Cuba, Gladys Bejarano na kumhakikishia ufunguzi wa Ofisi
za ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Aidha Majaliwa alisema kuwa Tanzania inatambua na kuthamini
mahusiano mazuri ya kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi, kielimu, kiafya na
kiutamaduni kati yake na Cuba hivyo inatarajia kufungua ubalozi nchini humo ili
kuweza kurahisisha utendaji wa kazi za kibalozi.
Waziri Mkuu huyo alikutana na Makamu huyo wa Rais jana wakati
alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi nchini Cuba ambapo malengo ya ziara
hiyo yalikuwa ni kuimarisha na kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
“Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati Tanzania na Cuba
ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba
wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, hivyo lazima tufungue ofisi za ubalozi
na tutamleta balozi wetu hapa”, alisema.
Pia aliishukuru Serikali ya Cuba kwa ujenzi wa kiwanda cha
dawa za kuua vijidudu vya maralia pamoja na ufadhili wa masomo ya udaktari
inaoutoa kwa wanafunzi wa Kitanzania ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali
nchini humo.
Vilevile aliiomba Serikali hiyo iendelee kutoa ufadhili wa
masomo kwa madaktari hao hadi ngazi ya shahada ya uzamili kwa sababu Serikali
ya Tanzania inawahitaji madaktari bingwa wengi kwani waliopo sasa ni wachache.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Gladys alimshukuru Waziri
Mkuu Majaliwa kwa kufanya ziara nchini Cuba na kumhakikishia kwamba uhusiano wa
Serikali yake na ya Tanzania utaendelea kuimarishwa kwa manufaa ya wananchi wa
pande zote mbili.
Alisema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dokta John
Magufuli inafanya jitihada kubwa ya kuhakikisha uchumi wake unakua kwa kasi
jambo ambalo ni tofauti na mataifa mengine.
Makamu huyo wa Rais aliongeza kuwa wataendelea kushirikiana katika
uboreshaji wa Sekta ya afya, utamaduni, kilimo, uchumi na elimu na kwamba kuhusiana
na ombi la kuongeza ufadhili wa shahada ya uzamili kwa madaktari alisema alilipokea
na kueleza kuwa atalifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment