Ziwa Nyasa. |
Na Julius Konala,
Nyasa.
MKUU wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Isabella Chilumba
amelipongeza shirika lisilo la kiserikali la Wasaidizi wa Sheria na Haki za
Binadamu (WASHEHABINYA) wilayani humo kwa kuendesha mafunzo juu ya utawala bora
kwa wananchi pamoja na viongozi wa vijiji na kata, ambayo yameweza kuwajengea
uwezo namna ya kuishi na kufanya shughuli zao za kimaendeleo.
Aidha mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tatu katika kata nne
za wilaya hiyo ambayo yamefadhiliwa na shirika la The Foundation For Civil
Society (FCS) kutoka Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa wilaya hiyo, Chilumba ndiye aliyefungua mafunzo hayo
juzi mjini hapa yaliyoshirikisha baadhi ya wananchi, wenyeviti wa vitongoji, vijiji,
pamoja na maofisa watendaji wa kata.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu huyo wa
wilaya alisema kuwa mradi huo umefika wakati muafaka kwa kile alichoeleza kuwa
wananchi wengi hawajui haki zao za msingi, kutokana na kutojua sheria pamoja na
kushindwa kesi zao mbalimbali Mahakamani kwa sababu ya ukosefu wa msaada wa
kisheria.
Chilumba alisema kuwa kutokana na baadhi ya wananchi na
watendaji wilayani humo kutojua sheria wamekuwa wakikiuka taratibu
mbalimbali ikiwemo kufanya uchafuzi wa mazingira, kwa kuosha magari na pikipiki
zao ufukweni mwa ziwa Nyasa hali ambayo inasababisha mafuta ya vyombo hivyo vya
moto kuchanganyika na maji na kupelekea upatikanaji wa samaki ndani ya
ziwa hilo kuwa mgumu.
Katika kukabiliana na tatizo hilo Mkuu huyo wa wilaya
amewataka pia washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia na kufuatilia kwa
umakini mada walizofundishwa na wakufunzi hao ili waweze kuboresha utendaji
kazi wao pamoja na kuwajengea uwezo wa jinsi ya ufuatiliaji wa rasilimali za taifa.
Awali Mratibu wa shirika hilo, Jacob Ngonyani akitoa taarifa
ya mradi huo kwa Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Chilumba alieleza kuwa Wasaidizi hao wa
sheria na haki za binadamu ni asasi ambayo ipo katika mchakato wa kutekeleza
sera ya taifa ya maendeleo hivyo wametekeleza mradi huo katika kata nne za wilaya
hiyo.
Ngonyani alizitaja kata zitakazonufaika na mradi huo kuwa ni
kata ya Kilosa, Mbamba bay, Lipingo pamoja na kata ya Liuli ambapo amedai kuwa
dhumuni la shirika hilo ni kutoa elimu ya sheria na haki za binadamu, kutoa
msaada wa kisheria kwa jamii, jinsi ya ufuatiliaji wa matukio ya ukiukwaji wa
haki za binadamu, kutoa ushauri na kusimamia haki za waathirika waishio na Virusi
Vya Ukimwi (VVU), kushirikiana na taasisi nyingine ndani na nje ya nchi na
kufanya utafiti.
Aliongeza kuwa pia hutoa elimu juu ya masuala ya usawa wa
kijinsia, afya ya jamii, utawala bora, umaskini wa kipato, mazingira, kilimo, utamaduni,
vijana wanawake na watoto huku akidai kuwa dhamira ya shirika hilo ni
kuhakikisha jamii inajengewa pia uwezo katika masuala ya sheria na haki za binadamu.
Naye mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo Mnung’a Mnung’a
alisema kuwa ili Tanzania iweze kufikia malengo iliyojiwekea ni lazima kazi na
nguvu za pamoja zitumike katika kujenga uchumi pamoja na ushirikishwaji wa
sekta mbalimbali.
Mnung’a alifafanua kuwa sababu kubwa iliyosababisha kuchelewa
kufikiwa kwa dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 ni ukosefu wa usimamizi
wa rasilimali mbalimbali za taifa, wananchi kutowajibika pamoja na kukithiri kwa
ubadhirifu serikalini jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha
nyuma maendeleo ndani ya nchi.
Aidha mwezeshaji mwingine, Wilgis Komba alibainisha kuwa ili
Tanzania iweze kufikia dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 watumishi wa
umma wanatakiwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uaminifu, kuepuka ubinafsi, uwajibikaji,
uwazi, kuheshimu sheria pamoja na kuacha vitendo vya upendeleo.
Komba aliwataka viongozi kutumia hekima na busara pindi
wanapotimiza majukumu yao, kuzingatia utii wa sheria, watumishi kuzingatia
maadili ya utumishi wa umma pamoja na wananchi kuwajibika ipasavyo badala ya kutegemea
kila kitu wafanyiwe na serikali.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Vailet Nkondola
alilipongeza shirika hilo la WASHEHABINYA kwa kuwajengea uwezo wa masuala ya utawala
bora huku akiliomba waendelee kuongeza wigo wa mradi huo, ili uweze kuwafikia
wananchi wengi waishio vijijini ambao bado hawajui namna ya kupata haki zao za
msingi.
No comments:
Post a Comment