Na Muhidin Amri,
Songea.
IMEELEZWA kuwa wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma, wapo hatarini kuugua magonjwa yatokanayo na mifugo ikiwemo ugonjwa wa
majipu na TB baada ya kubainika kwamba, baadhi ya wafanyabiashara wachache
wamekuwa wakichinja na kuuza nyama bila kukaguliwa na madaktari wa mifugo.
Hayo yalisemwa juzi na mkaguzi wa mifugo katika
machinjio ya Msamala katika Manispaa hiyo, Angela Mbata wakati alipokuwa akitoa
elimu ya mifugo na umuhimu wa kula nyama iliyopimwa kwa wananchi waliohudhuria
kwenye maonesho ya wakulima maarufu kwa jina la nanenane mkoani hapa
yaliyofanyika katika kata ya Masamala.
Mbata alifafanua kuwa uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa
ng’ombe 15 kati ya 30 wanaoletwa na wafugaji mkoani humo kutoka katika mikoa
mbalimbali kwa ajili ya kuchinjwa, imebainika kuwa na ugonjwa wa minyoo kwenye
ini na mapafu ambayo husababisha majipu jambo ambalo ni hatari kubwa kwa
walaji.
Alisema kuwa binadamu atakayekula nyama hasa maini na
mapafu ya wanayama waliokuwa na ugonjwa huo ni rahisi na yeye kuambukizwa na
kwamba tatizo hilo linatokana na mifugo kutotibiwa kwa muda mrefu hasa ile
inayotoka kwenye mnada wa Mbeya ambapo wafugaji wanasafirisha mifugo yao
kupitia njia za panya.
Aidha aliongeza kwa kuwatahadharisha wananchi kuwa
makini na kuepuka kununua na kula nyama mitaani kwa sababu mifugo inayochinjwa
katika maeneo yao wakati mwingine sio salama kwa kuwa haikaguliwi na madaktari
wa mifugo wakiwa na lengo la kuepuka gharama.
Alibainisha kuwa katika kuwanusuru wananchi waishi
katika Manispaa ya Songea wamejipanga kuhakikisha mifugo yote inayoingia ikitoka
nje ya Manispaa hiyo ni lazima ikaguliwe kwanza, kabla ya kupeleka kwenye
minada kwani wasipofanya hivyo inaweza kuleta madhara makubwa kwa binadamu na hatimaye
kushindwa kushiriki vyema katika shughuli za ujenzi wa taifa.
Kadhalika alisema serikali imejipanga kuhakikisha kwamba
hakuna ng’ombe atakayechinjwa bila kukaguliwa na daktari ambapo mfugaji au
mfanyabiashara yeyote atakayeingiza au kuuza nyama isiyopimwa atapewa adhabu kali
ikiwemo kufikishwa Mahakamani kupigwa faini na kwenda kutumikia kifungo jela.
Hata hivyo Mbata alibainisha kuwa tatizo la wananchi hasa
wakulima wa mkoa wa Ruvuma ni kutopenda kuhudhuria na kushiriki kikamilifu
maonesho mbalimbali ya wakulima ambayo yanaweza kuwasaidia kupata elimu kuhusu
ufugaji wa kisasa, kilimo bora na ulaji wa vyakula unaozingatia kanuni bora za
afya.
No comments:
Post a Comment