Wachimbaji wa madini wakiwa katika mto Lunyere Darpori wakisafisha mchanga wenye madini. |
Hili ni eneo moja wapo la mto Lunyere Darpori ambalo tayari limeharibiwa na wachimbaji hao. |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
TAASISI ya maji ya Water Laboratory unity na Chemical and
Environmental services za Jijini Dar es Salaam, wamebaini kuwa mto wa Lunyere
uliopo katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma una kiwango kikubwa cha kemikali
aina ya Zebaki (Mercury) ambazo ni hatari kwa viumbe hai.
Zebaki hiyo hivi sasa imefikia kipimo cha Hg/ug 0.02 kiwango ambacho
hakikubaliki kitaifa na kimataifa kwa kuwa kina madhara makubwa kwa viumbe
hivyo.
Utafiti huo uliofanywa na taasisi hizo unaeleza kuwa Zebaki
hiyo imefikia hatua ya kuendelea kuingia katika mto Ruvuma hadi katika bahari
ya Hindi.
Kwa ujumla mto
Lunyere umekuwa ukichafuliwa na wachimbaji wa madini waliopo kwenye eneo la
Darpori mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambao huko huchimba madini ya aina
mbalimbali hali ambayo inasababisha hata mto Ruvuma na maeneo mengine
kuathirika zaidi.
Wataalamu
wamekuwa wakisisitiza siku zote kuwa kamwe mtu asiiguse Zebaki kwa kula kupitia
chakula au maji kwani ikiguswa inaingia moja kwa moja mwilini kwenye damu na
inakwenda kutua kwenye ubongo na kusababisha ubongo kusimama hivyo kushindwa
kufanya kazi yake ipasavyo.
Vilevile
kemikali hiyo ikisha ingia mwilini mwa binadamu imekuwa ikileta madhara ikiwemo
magonjwa kama vile saratani, ulemavu wa akili na hatimaye kifo.
Pia wataalamu wanatahadharisha kuwa ukila
samaki wanne tu wenye Zebaki unaweza kuathirika na madhara hayo huchukua miaka
mingi kujitokeza ndiyo maana ni vigumu kwa binadamu kutambua kwa haraka kwamba
alipata matatizo hayo lini baada ya kutumia bidhaa ambazo zimeathirika na kemikali
hiyo.
No comments:
Post a Comment